01 August 2013

VIGOGO MAGEREZA WATIMULIWA KAZINa Grace Ndossa
 MKUU wa Gereza la Kiteto na Mrakibu Msaidizi wa Magereza wamefukuzwa kazi kutokana na kukamatwa na Kikosi cha Kuzuia Ujangili Kanda ya Kati wakiwa na nyara za serikali.Maofisa hao waliofukuzwa kazi ni Mrakibu wa Magereza, Ally Ramadhani Sauko ambaye kabla ya tukio hilo alikuwa Mkuu wa Gereza la Kiteto na Msaidizi wake Mrakibu Msaidizi wa Megereza, Joseph Kimaro.

  Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Isaac Nantanga, alieleza kuwa maofisa hao wamefukuzwa kazi kutokana na kukamatwa na nyara za serikali kuanzia Julai 23, mwaka huu."Katibu Mkuu wa Wizara ya mambo ya ndani ya nchi amewafukuza kazi kwa kutumia madaraka aliyopewa chini ya kifungu cha 34 (6) cha kanuni za utumishi wa magereza wa mwaka 1997," alisema Nantanga.
  Pia alisema kufukuzwa kwa maofisa hao ni kutokana na matumizi mabaya ya madaraka kwa kuruhusu mali za serikali, ikiwemo gari na silaha kutumika kuua wanyama.Wakati huo huo, alisema serikali iko katika mchakato wa kuwatafutia suluhisho la kudumu wakimbizi 173,763 ambao wako katika makazi ya wakimbizi ya Mishamo, Katumba Wilayani Mpanda mkoani Katavi na Ulyankulu mkoani Tabora ambao waliingia nchini miaka ya 1970 na walipewa makazi hayo ambayo walikuwa wanajitegemea.  
Pia alisema wakimbizi wengine 2,117 kutoka Somalia ambao wana asili ya Kibantu waliopo katika makazi ya Chogo Tanga nao wanatafutiwa suluhisho la kudumu kuhusiana na uwepo wao nchini ambao waliingia nchini mwaka 1990 baada ya kutokea kwa machafuko nchini kwao."Pale wakimbizi hawawezi kurejeshwa kwao au kupewa uraia, ufumbuzi mwingine ni kuwapeleka nchi nyingine ambapo jumla ya wakimbizi 14,000 wa Burundi walipelekwa nchini Marekani, lengo la Serikali ni kuona suala la wakimbizi hapa nchini linafikia tamati,"alisema Nantanga. Hata hivyo alisema Serikali imefanikiwa kuwarejesha kwao wakimbizi pamoja na kufunga kambi 12 kati ya 13 za wakimbizi zilizopo hapa nchini zilifungwa kuanzia mwaka 2007 hadi 2013.  
Alisema kambi ambayo imebaki ni ya Nyarugusu iliyoko Kasulu Mkoani Kigoma ambayo inahifadhi wakimbizi kutoka Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo 63,728 kutoka Burundi 4,153 na nchi nyingine za Kiafrika 212.Hata hivyo alisema kuwa kambi ya Nyarugusu itafungwa baada ya wakimbizi waliopo kurejeshwa kwao pale hali ya usalama nchini kwao itakapoimarika.

No comments:

Post a Comment