01 August 2013

MKANDARASI KUBURUTWA KORTINI



Na Yusuph Mussa, Handeni
BAADHI ya Madiwani wa Halmashauri ya Mji Handeni mkoani Tanga wametaka mkandarasi aliyekuwa anajenga barabara za mji wa Handeni zenye urefu wa kilomita 11 akamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa madai amelipwa fedha wakati amejenga chini ya kiwango.

Akizungumza mwishoni mwa wiki kwenye Baraza la Halmashauri ya Mji Handeni, Diwani wa Kata ya Vibaoni, Mhandisi Mkusa Nkondo alisema kuna uzembe umefanyika katika kumlipa mkandarasi huyo fedha za kazi hiyo kwa asilimia 99 wakati hakustahili.
"Mkandarasi anayejenga barabara za mji wa Handeni hakustahili kulipwa fedha hizo kwa vile amejenga chini ya kiwango, lakini kibaya zaidi ni kwa nini amekimbilia kulipwa kwa karibu asilimia 99 ya fedha zote. Maana alikuwa afanye kazi hii kwa sh. milioni 75 na amelipwa sh. milioni 71.
"Tunaomba madiwani tupitishe azimio mkandarasi huyu akamatwe ili aweze kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa kuchukua fedha ambazo hajazifanyia kazi. Huyu ni mwizi fedha zimetoka na kazi hajafanya. Ina maana hizi sh. milioni tatu zilizobaki anaweza kufidia kwa kazi ambayo hajafanya" alisema Mhandisi Nkondo.
Kaimu Mhandisi wa Halmashauri ya Mji wa Handeni, Joachim Mmbaga alisema alikuwa anaandika malipo ya mkandarasi huyo kwa shinikizo la Mhandisi wa Ujenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni aliyefahamika kwa jina moja la Isangura.
"Nilikuwa naandika cheti cha malipo kwa mkandarasi kwa kushinikizwa. Lakini nilikuwa naambiwa ni haki mkandarasi huyo kulipwa kwa vile barabara alizokuwa anatakiwa kuzifanyia ukarabati ni zenye upana wa mita sita, lakini akawa anatengeneza barabara zenye mita 10, hivyo moramu yake ilikuwa anasambaza zaidi hivyo kuonekana chini ya kiwango," alisema Mmbaga.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Handeni, Thomas Mzinga alisema ni mapema mno kumchukulia hatua za kisheria mkandarasi huyo hadi hapo watakapopitia taarifa za kazi zake na baada ya hapo watajua hatua za kuchukua.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Dkt. Khalfany Haule, ambapo halmashauri yake ndiyo iliingia mkataba wa kutengeneza barabara hizo kwa kiwango cha changarawe, alisema ofisi yake ni lazima ifuatilie suala hilo na baada ya kupata majibu watawajulisha madiwani na wajumbe wa baraza hilo.
Akizungumza kwa simu na mwandishi wa habari hizi akiwa jijini Dar es Salaam, mkandarasi wa kampuni iliyojenga barabara hizo ya Summer Tec Ltd aliyejitambulisha kwa jina moja la Robert alisema malipo aliyopewa ni halali na yupo tayari kuitwa na kuhojiwa.
"Mimi nimefanya kazi kwa mujibu wa sheria na inajulikana wazi barabara niliyokuwa najenga upana wake uliongezeka karibu mita nne, hivyo kufanya kazi kuwa ngumu, lakini nilifanya kwa ufanisi, ila kwa vile sijakabidhi kama kuna sehemu itakuwa na kasoro nitarekebisha," alisema Robert.
Naye Mhandisi Isangura akizungumza kwa njia ya simu na mwandishi wa habari hizi baada ya kuhamishwa kwenye wilaya hiyo, alisema hakumshinikiza Mmbaga kuidhinisha malipo ya mkandarasi, bali walikuwa wanalipa baada ya kujihakikishia kuwa kiwango kilichotengenezwa kinastahili malipo.  

No comments:

Post a Comment