01 August 2013

MAWAZIRI WATEMA CHECHE KANDA YA ZIWA



Na Benard Bugoma
WAZIRI wa Nishati n a Ma d i n i , P r o f . S o s p e t e r Mu h o n g o a m e w a h a k i k i s h i a wananchi wa Chato kupatikana kwa umeme wa uhakika kabla ya mwisho wa mwaka huu.Waziri Muhongo alieleza kwamba wizara yake kupitia Shirika la Umeme (TANESCO) imekamilisha ununuzi wa jenereta lenye uwezo wa MVA 1.2 kwa ajili ya matumizi ya Wilaya ya Chato.

Alisema Mji wa Chato na vitongoji vyake umekuwa na tatizo la muda mrefu la kukatika umeme mara kwa mara kutokana na kuchakaa na kuzidiwa nguvu kwa jenereta zinazotumika sasa ambazo zimefungwa wilayani Biharamulo."Jenereta mbili zilizopo zinauwezo wa MVA 0.8 zote kwa pamoja na zinahudumia wilaya mbili za Biharamulo na Chato, kwa sasa uwezo wa jenereta hizo hautoshelezi mahitaji ya umeme ambayo yanaongezeka kwa kasi," alisema Muhongo
Waziri Muhongo alisisitiza kuwa hadi ifikapo Novemba mwaka huu jenereta hiyo mpya kwa ajili ya Wilaya ya Chato itakuwa imewasili.Alitoa kauli hiyo wakati akihutubia katika mkutano wa hadhara uliojumuisha mawaziri watatu walioandamana kukagua shughuli za maendeleo katika Jimbo la Chato.
Mawaziri wengine waliokuwapo katika mkutano huo ni pamoja na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Prof. Anna Tibaijuka na Waziri wa Kilimo na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiza.Kuhusu matatizo ya upatikanaji wa pembejeo za kilimo, Waziri Chiza aliwataka wananchi wa Chato kuwasilisha maombi yao kwa ajili ya mikopo ya kununulia zana za kilimo na hasa matrekta.
Waziri Chiza alielezea kuwa fursa ya kupata mikopo hiyo ni kwa wananchi wote, hivyo a l iwa h ama s i s h a wa n a n c h i hao kupitia kwa Mbunge wao kutopoteza nafasi hiyo ambayo yeye pia atafuatilia utekelezaji wake.Kwa upande wake Waziri wa Ardhi, Prof. Tibaijuka amekemea tabia ya baadhi ya wananchi kukodi maeneo makubwa ya ardhi ambayo huyatumia kuwakodisha wakulima wadogo wadogo.
Waziri Tibaijuka alielezea kuwepo kwa mtindo kwa baadhi ya wenyeviti wa halmashauri kujichukulia madaraka na kuanza kugawa viwanja kinyume na taratibu hali ambayo inatoa mwanya kwa watu wachache wasio waaminifu kuhodhi maeneo makubwa kwa lengo la kuwakodisha wakulima wadogo wadogo ambao kutokana na ukiritimba hujikuta wanashindwa kupata maeneo ya kilimo karibu na vijiji vyao.
Aidha waziri huyo aliahidi kutoa fedha kwa ajili ya kuchangia juhudi za halmashauri za kupima viwanja ili wananchi wa kawaida nao waweze kupata fursa hiyo ya kumiliki maeneo yao badala ya kuendelea kutumia mashamba ya kukodi ambayo huwaumiza kiuchumi.
Akihitimisha mkutano huo Waziri wa Ujenzi ambaye pia ndiye Mbunge wa jimbo hilo la Chato Dkt. John Magufuli aliwashukuru mawaziri hao kwa kulitembelea jimbo lake na kuweza kugusa kero ambazo zimekuwa zikiwasumbua wananchi wa Chato kwa muda mrefu.  

No comments:

Post a Comment