Na Suleiman Abeid,
Meatu
BARAZA la madiwani
katika halmashauri ya Wilaya ya Meatu Mkoa wa Simiyu limemwagiza mkurugenzi
mtendaji wa halmashauri hiyo, John Wanga kufanya kila linalowezekana ili kuwezesha
kununuliwa kwa kipimo cha kupimia sampuli za damu (CD.4) katika hospitali ya
wilaya.
Agizo hilo limetolewa
juzi na madiwani wakati wa kikao chao cha kufunga mwaka wa fedha ambapo
walishitushwa na taarifa iliyotolewa katika kikao hicho na Mwenyekiti wa Kamati
ya Kudhibiti UKIMWI kwamba hospitali ya wilaya haina kifaa cha kupimia CD.4 na
hulazimika kupeleka kupima sampuli za damu wilayani Kishapu.
Kwa mujibu wa taarifa
iliyotolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya UKIMWI, Basu Kayungilo, mashine ya
kupimia CD.4 katika hospitali ya Wilaya ya Meatu iliharibika kipindi kirefu
kilichopita ambapo hivi sasa uongozi wa hospitali hiyo hulazimika kupeleka
sampuli za damu wilayani Kishapu kwa ajili ya upimaji.
Taarifa hiyo
ilifafanua kuwa tatizo lililochangia mashine hiyo kutofanyiwa matengenezo
mapema ni ukosefu wa 'spea' zake na kwamba hata hivyo kazi ya ukarabati hupaswa
kufanywa na wazabuni waliofunga mkataba na wizara ya afya hali ambayo huchukua
muda mrefu kwa kazi kufanyika.
"Mheshimiwa
mwenyekiti wilaya yetu hivi sasa inalazimika kupeleka sampuli za damu wilaya ya
jirani ya Kishapu kwa ajili ya upimaji ili kuhakikisha damu inayotumika kwa
wagonjwa ni damu salama, hali hii ni kutokana na mashine yetu ya CD.4 katika
hospitali ya wilaya kuharibika kwa muda mrefu sasa."
"Hali hii ni
hatari kwa usalama wa wakazi wetu, hata hivyo urasimu wa wizara ndiyo
uliochangia mashine hiyo isikarabatiwe mapema, japokuwa tumeahidiwa kwamba
tayari fedha zimepatikana kiasi cha shilingi milioni nne na mwezi ujao kazi ya
ukarabati inaweza kuwa imekamilika," alieleza Kayungilo.
Hata hivyo pamoja na
taarifa ya mwenyekiti huyo madiwani hao kwa kauli moja waliagiza kununuliwa kwa
mashine mpya badala ya kutegemea mbovu na kumwagiza mkurugenzi kufanya chini
juu ili mashine hiyo iweze kununuliwa mapema.
Akijibu agizo hilo,
mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Wanga alisema suala la kipimo cha damu
salama katika hospitali ya wilaya ni la muhimu na kwamba atawasiliana na Katibu
Tawala wa Mkoa (RAS) ili kuanza mchakato wa kupata mashine mpya ya CD.4 hivi
karibuni.
Kwa upande mwingine madiwani hao waliagiza
kufanyika kwa ukarabati wa vifaa vyote vya upimaji vilivyopo katika hospitali
hiyo, vituo vya afya na zahanati ili viweze kufanya kazi kama kawaida kwa lengo
la kuwaondolea kero wakazi wa wilaya hiyo kuhangaika katika vituo vya watu
binafsi
No comments:
Post a Comment