02 August 2013

CHINA YATOA DAWA ZA MALARIA NCHINI Leah Daudi Na Penina Malundo
SERIKALI ya China imekabidhi dawa za malaria zenye thamani ya sh. bilioni mbili kwa Serikali ya Tanzania ambazo zitasaidia kutibu ugonjwa huo hapa nchini.Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wakisaini mkataba huo Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Hussein Mwinyi alisema kuwa amepokea dawa hizo aina ya ANTI-MALARIA kutoka katika Serikali ya China ambapo zina uwezo mkubwa wa kutibu ugonjwa huo.

Alisema kuwa, Serikali ya China kwa kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imekabidhi dawa hizo ambazo zitasaidia katika ungonjwa wa malaria ambao umekuwa ni tishio hapa nchini."Tangu mwaka 1968 Serikali ya China imekuwa ikiisaidia Tanzania katika sekta ya afya kwa mambo mengi, ikiwa ni pamoja na kufundisha wataalamu na kupata ujuzi katika sekta hiyo," alisema Dkt. Mwinyi.
Hata hivyo alisema, awali Serikali ya China ilileta wataalamu wake zaidi ya 2,000 na kusambazwa sehemu mbalimbali nchini kwa ajili ya kufanya kazi katika sekta ya afya.Alisema, China imesaidia katika ujenzi wa jengo la matibabu katika Kitengo cha Moyo kilichopo Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Naye Balozi wa China hapa nchini, Lu Youqing alisema kuwa tangu mwaka 2006 hadi 2012 China imeweza kuchangia dozi 400,000 na sindano zenye thamani ya sh. bilioni nne.Alisema, kwa kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii hapa nchini msaada huo uliweza kusambazwa zaidi ya hospitali 100.

No comments:

Post a Comment