02 August 2013

MADIWANI WAPINGA AGIZO LA RCNa Suleiman Abeid, Simiyu
BAADHI ya madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu wamepinga agizo lililotolewa na Mkuu wa Mkoa huo, Paschal Mabiti lililozitaka halmashauri za wilaya kutowazuia wanunuzi wa pamba wenye madeni ya ushuru wa zao hilo na kuagiza wapewe leseni.

Wakizungumza na Majira juzi mjini Mwanhuzi madiwani hao walielezea kushangazwa kwao na agizo la mkuu huyo wa mkoa ambalo walidai amelitoa kwa kulalia upande mmoja wa matajiri bila kujali masilahi ya halmashauri za wilaya ambazo yeye ndiye mlezi wake.
Walisema wao binafsi katika halmashauri ya Meatu hawako tayari kumpatia leseni mnunuzi wa zao la pamba ambaye anadaiwa deni la miaka ya nyuma la ushuru huo na kwamba kulazimisha wanunuzi hao ambao ni wadaiwa sugu waruhusiwe kununua pamba katika wilaya hiyo ni sawa na kuongeza mzigo wa deni.
"Huyu mkuu wa mkoa tunafikiri aidha alipitiwa tu wakati anatoa agizo hilo, sisi hata mwaka jana aliposhinikiza wanunuzi waruhusiwe kununua pamba bila ya kulipia kwanza ushuru, tulimgomea, wengi walilipa tukawaruhusu, leo tena kaibuka na hoja nyingine ya kutaka kuwasaidia wadaiwa sugu tunasema hilo haliwezekani,"
"Sisi ndiyo wenye halmashauri hii, ndiyo tunaopaswa kuhakikisha ma p a t o y a h a lma s h a u r i yanakusanywa kwa wingi ili kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo tuliyojipangia, leo anataka kuwabeba matajiri huku halmashauri zikihangaika kutafuta mapato yake, hatufanyi hivyo," alieleza Diwani Chalya Seni.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kisesa (CCM), Luhaga Mpina alisema agizo la mkuu huyo wa mkoa halitekelezeki na kwamba ni vizuri kwanza angewashawishi matajiri wote wanaodaiwa na halmashauri za wilaya walipe madeni yao badala ya kuzitaka halmashauri ziwavumilie na kuendelea kuwapa leseni za ununuzi.
"Ha iwe z e k a n i mt u a n a malimbikizo ya madeni aendelee kuruhusiwa kununua pamba katika halmashauri yetu, halmashauri zinahitaji mapato, suala la kutaka tuwavumilie halipo, hapa kwetu hatutaruhusu mnunuzi yeyote anayedaiwa deni la ushuru wa nyuma aendelee kununua pamba, ni mpaka pale atakapokuwa ametulipa," alieleza Mpina.
Mapema wiki iliyopita alipokuwa akifungua kikao maalumu cha baraza la madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Bariadi kilichoitishwa kwa ajili ya kugawana mali kati ya halmashauri hiyo na ile ya Itilima (mpya), Mabiti aliziagiza halmashauri zote kutowanyima leseni za kununulia pamba wanunuzi wanaodaiwa madeni ya nyuma ya ushuru.
Mabiti alisema licha ya kuwa wanunuzi hao wana madeni makubwa na wengine kufikishwa mahakamani wakishtakiwa kwa kushindwa kulipa madeni hayo isiwe kigezo cha kuwawekea vizuizi na kuwanyima leseni kwa ajili ya ununuzi wa pamba kwa msimu wa mwaka huu.

No comments:

Post a Comment