06 August 2013

MAZITO BANDARI


Na Salim Nyomolelo
MAMLAKA ya Bandari Tanzania (TPA), imeingia kwenye mvutano na baadhi ya wadau wake kutokana na kuingia mkataba na kampuni ya kigeni itakayokuwa inaratibu mfumo wa Electronic Cargo Tracking Note System (ECTN) kwa mizigo inayoingia nchini kupitia bandari ya Dar es Salaam, pasipo kuwashirikisha.

Mbali na kutowashirikisha wadau hao, menejimenti ya TPA inadaiwa kukwepa kuhudhuria vikao viwili vilivyoitishwa na SUMATRA na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali, baada ya tangazo la kuanzishwa kwa mfumo huo kutangazwa kwenye vyombo vya habari.
Katika tangazo la TPA kwa vyombo vya habari la Julai 12, mwaka huu lilieleza kuwa kuanzia Septemba Mosi mwaka huu, mizigo yote itakayoingia nchini kupitia bandari hiyo itakuwa inapitia mfumohuo wa Electronic Cargo Tracking Note System (ECTN).
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari muingizaji wa mizigo atatakiwa kulipa ada kwa ajili ECTN Euro 50 sawa na sh. 104,500, mbali na gharama ndogo ndogo ambazo hazijajulikana.
“Hii itatugharimu muda na fedha nyingi ambazo hazijajulikana,” kilisema chanzo chetu.
Vyanzo vyetu vilidai kuwa Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Madeni Kipande, alikubali kuingia makubaliano na kampuni moja ya nje (jina tunalo) kusimamia mfumo wa ECTN, bila ya kuwasiliana na mamlaka nyingine husika ikiwa ni pamoja na SUMATRA.
Chanzo hicho kilisema kuwa kazi ya msingi katika shughuli za mamlaka ya bandari ni kupokea makontena na magari, kuhifadhi katika usalama kwa niaba ya makampuni ya Meli zinazoingiza mizigo, hadi pale nyaraka zitakapotolewa kwa ajili ya kuitoa mizigo hiyo baada ya kulipa tozo za uhifadhi, ni kwa faida ya nani mamlaka ya bandari inataka ECTN na nani aliwapa jukumu la kufanya hili? alihoji
Chanzo hicho kiliendelea kuhoji kuwa kuna gharama gani inayohusishwa na mfumo huu? Kama jibu ni ndio mbona hakuna jedwali la tozo lililowasilishwa kwa SUMATRA na kupitishwa bila ya kusainiana mkataba?
“Baada ya kutolewa kwa tangazo hilo TPA, SUMATRA waliitisha mikutano miwili na kuwataarifu wadau ambapo licha ya TPA kupata taarifa, lakini walishindwa kuhudhuria wakati wao (TPA) ndiyo walipendekeza siku na muda wa kikao cha pili, naona waligundua makosa yao ndio maana walishindwa kufika,” kilisema chanzo na kuongeza;
“Kama taratibu zote zingefuatwa, je ECTN ingehitajika? Na je, itaongeza tija kwa TPA, Taifa, au uagizaji wa mizigo?
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu mfumo huo unadaiwa kutokuwa na manufaa yoyote zaidi kwa sababu utahamisha fedha nyingi kutoka Tanzania kwenda anayeratibu mfumo huo (kampuni iliyoingia mkataba na TPA) kutokana na kulipwa Euro 50 kwa kila mzigo.
Habari za ndani zinaeleza Julai 22, mwaka huu SUMATRA iliitisha mkutano wa wadau wote ikiwa ni pamoja na TAFFA, TASAA, Shippers Council, TCCIA, TRA na TPA ili kujadili mfumo wa ECTN, lakini mkurugenzi wa TPA hakufika.
Vyanzo hivyo zinaeleza kuwa alipopigiwa simu inadaiwa kwamba, alidai kuwa yupo kwenye foleni anaelekea kwenye hicho kikao, lakini hakufika kabisa.
Mwingine ambaye hakuhudhuria mkutano huo muhimu ni Kamishna wa Ushuru wa Forodha wa TRA, ambapo alitoa udhuru.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, baada ya kumalizika kikao, Mkurugenzi Mkuu wa SUMATRA aliwaomba wanachama kuwa na subira wakati Mamlaka ikiendelea kuchunguza suala hilo.
Gazeti lilipomtafuta, Kipande jana ili atolee ufafanuzi madai hayo, alimwelekeza mwandishi wa habari hizi aonane na Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa TPA, Phares Magesa, ili atoe ufafanuzi huo.
Magesa alisema mfumo huo utasaidia kuongeza biashara na mapato kwa taifa kutokana na mizigo na meli kutokaa muda mrefu bandarini.
Magesa alisema mfumo huo utasaidia kuharakisha utoaji wa mizigo bandarini pamoja na kuokoa muda wa meli kusubiria upakuaji wa mizigo kwani taarifa zote zitakuwepo.
Pia alisema utapunguza gharama za kuhifadhi mizigo na meli kukaa kwa muda mrefu. Alisema ECTN itasaidia kuongeza usalama kwani ufuatiliaji utakuwepo tangu mzigo utakapopakiwa katika meli kutoka nchi husika.
Akizungumzia kuhusu gharama ya ECTN, alisema kuwa bado hazijajadiliwa, lakini kabla ya Septemba mwaka huu zitakuwa zimejulikana.
Kuhusu tuhuma zinazoikabili kampuni ambayo TPA imeingia nayo mkataba huo, Magesa alisema wao kama TPA hayo hayawahusu, isipokuwa inahusu kampuni yenyewe.
Kuhusu sababu za kuanzisha mfumo huo, alisema sheria ya Mamlaka ya Bandari namba 17 ya mwaka 2004 inaruhusu TPA kuingia mkataba na kampuni yoyote ili kuongeza ufanisi na kuongeza kuwa kuna mikataba mingi imesainiwa kupitia sheria hiyo.
Al i p o u l i zwa s a b a b u z a kutowashirikisha wadau wengine na kushindwa kuhudhuria mikutano, alisema; “Muda wa kushirikisha wadau hao haujafika, ukifika watafanya.”
Kuhusu kutohudhuria vikao, alisema walipata taarifa ambapo kikao cha kwanza walishindwa kuhudhuria kwani walikuwa na kikao na Benki ya Dunia (WB) na baada ya hapo walikutana na Baraza la Wafanyakazi kwa muda huo kikao kilichoitishwa na SUMATRA kilikuwa kinafanyika.
“Kikao cha pili nilichelewa kufika na nilitoa taarifa ambapo nilifika na wakaniona lakini waliamua kufunga kikao,” alisema Bw. Magesa kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, Kipande.
Ofisa Uhusiano wa Umma wa TRA, Oliver Njunwa, alipotakiwa kuzungumzia sakata hilo, alisema msemaji mkuu wa mamlaka hiyo amesafiri nje ya nchi na kwamba huyo, ndiye anaweza kuzungumzia suala hilo.
Juhudu za kupata Waziri wa Uchukuzi, Dkt. Harrison Mwakyembe, kuzungumzia suala hilo ziligonga mwamba.
No comments:

Post a Comment