02 August 2013

KILIMANJARO YAONGOZA KUIBA UMEMENa Florah Temba, Moshi
MKOA wa Kilimanjaro umetajwa kuongoza kwa wizi wa miundombinu ya umeme katika kanda ya Kaskazini, ambapo katika kipindi cha mwezi Julai mwaka huu, nyaya za umeme zenye urefu wa mita zaidi ya 3,750, zimeibiwa katika kata ya Kia wilaya ya Hai mkoani humo, na kusababisha hasara ya zaidi ya shilingi milion 50.

Katika kipindi cha Januari hadi Julai mwaka huu, shirika la umeme nchini Tanesco, Mkoa wa Kilimanjaro limepata hasara ya zaidi ya shilingi milioni 100 kutokana na wizi wa nyaya za umeme, hasara ambayo ni kubwa ikilinganishwa na mwaka jana ambapo katika kipindi cha Januari hadi Disemba zilipotea milioni 80 kutokana na wizi wa nyaya.
Hayo yalibainishwa jana na Meneja Mwandamizi wa Tanesco Kanda ya Kaskazini, Mhandisi Makoye Ng'erere wakati akitoa taarifa ya matukio ya wizi wa miundombinu ya umeme kwa waandishi wa habari mkoani hapa ambapo alisema katika kanda ya Kaskazini inayojumuisha Mkoa wa Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Tanga, mkoa wa Kilimanjaro unaongoza kwa matukio hayo ukifuatiwa na mkoa wa Arusha.
Mhandisi Ng'erere alisema katika kipindi cha Julai mwaka huu wizi wa miundombinu ya umeme katika Mkoa wa Kilimanjaro, umefanyika mara tatu mfululizo ambapo tukio la kwanza lilitokea Julai 13 na nyaya zenye urefu wa mita 750 ziliibwa, Julai 17 nyaya zenye urefu wa mita 1,000 na Julai 21nyaya zenye urefu wa mita 2,000 na kwamba matukio hayo yote yalitokea katika Kata ya Kia wilayani Hai.
"Matukio haya yanasababisha hasara kubwa kwa shirika hili, na hasara inayotokea si ya fedha tu ni pamoja na wananchi wanaohudumiwa na shirika hili katika maeneo ambayo yameibiwa nyaya kukosa umeme na kurusha lawama kwa Tanesko huku tatizo likiwa si letu, kukosekana kwa usalama kutokana na watu kutumia fursa ya kukosekana kwa umeme kufanya matukio ya uhalifu na shirika kupoteza heshima kwa wananchi kutokana na kukatika kwa umeme bila ya taarifa," alisema.
Mhandisi huyo alisema zipo jitihada mbalimbali ambazo tayari zimeshachukuliwa na Serikali ya Mkoa wa Kilimanjaro ili kudhibiti matukio hayo ya wizi wa miundombinu ya umeme, ikiwa ni pamoja na kuundwa kwa kamati ya kupambana na wahalifu hao.
Alisema kamati hiyo ambayo iliundwa baada ya kikao cha kamati ya ulinzi na usalama mkoani humo kukaa Julai 24 mwaka huu tayari imefanikisha kukamatwa kwa watu wanne wakiwa na nyaya za umeme ambazo hazikuweza kufahamika mara moja urefu wake, kutokana na kukatwa vipande vipande na kuwekwa kwenye mifuko ya 'Salfet' tayari kwa kusafirishwa.
Alisema watu hao ambao w a l i k a m a t w a n a n y a y a zinazosadikiwa kuibwa katika kata ya Kia wilaya ya Hai, walikamatwa Julai 26, mwaka huu katika eneo la Kiboroloni Manispaa ya Moshi na kwamba haijafahamika nyaya hizo walikuwa wakizisafirisha kwenda wapi.
Kufuatia kuendelea kushamiri kwa matukio ya wizi wa miundombinu ya umeme, shirika hilo kanda ya Kaskazini limetangaza zawadi ya shilingi 50,000 hadi milioni tano kwa mwananchi atakayetoa taarifa zitakazowezesha kukamatwa kwa watu wanaojihusisha na vitendo vya wizi na kuhujumu miundombinu ya umeme.
Akizungumza Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Robert Boaz, alikiri kukamatwa kwa watu wanne kwa tuhuma za kujihusisha na wizi wa nyaya za umeme.
Kamanda Boaz alisema watu hao ambao walikamatiwa mjini Moshi, bado wanashikiliwa na jeshi hilo na kwamba upelelezi bado unaendelea na pindi utakapokamilika hatua nyingine za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

No comments:

Post a Comment