01 August 2013

KASI YA USAMBAZAJI MAJI YAONGEZEKA



 Na Ramadhan Libenanga,
 MWENYEKITI wa Bodi ya Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA), Mtumwa Khatib Ameir amesema mamlaka hiyo imepiga hatua kubwa katika usambazaji wa maji safi na salama licha ya kasoro ndogo ndogo zinazojitokeza. Hayo aliyaeleza katika mkutano wa mwaka wa wafanyakazi wa ZAWA uliokwenda sambamba na kuwaaga wastaafu na kuwazawadia wafanyakazi bora, uliofanyika katika ukumbi wa mkutano wa Mamlaka hiyo uliopo Gulioni mjini Zanzibar.

Alisema kuwa pamoja na mafanikio hayo lakini bado wafanyakazi hao wanapaswa kuongeza bidii katika utendaji wao wa kazi ili kuweza kuendelea kutoa huduma bora kwa jamii.Alisema kuwa hatua hiyo haitasaidia utoaji wa huduma bora pekee bali itapelekea kuondoa kasoro hizo hasa ikizingatiwa kuwa sekta hiyo ndio tegemeo kubwa kwa jamii iliyowazunguka.
"Msitosheke na hapa mlipofika ni vyema mkaongeza bidii katika kuziondoa kasoro hizi kwani sekta ya maji ni muhimu kwa maisha ya wananchi," alisema. Sambamba na hilo Mwenyekiti huyo alisema uongozi wa ZAWA kupitia bodi yake utashirikiana na wafanyakazi hao katika kukabiliana na matatizo ikiwemo uimarishaji wa maslahi yao. Kwa upande wao wafanyakazi hao wameuomba uongozi wa mamlaka ya maji kuzingatia mazingira ya usalama kazini kwani wanafanya kazi nzito na za hatari bila ya kuwa na kinga na vifaa vya usalama

No comments:

Post a Comment