01 August 2013

BARABARA ZAKARABATIWA KILAKALA



Morogoro

DIWANI wa Kata ya Kilakala, Ribon Mkali ameipongeza halmashauri hiyo kwa kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM kwa kuhakikisha wanachonga barabara zote za kata hiyo ambazo awali zilikuwa hazipitiki. Diwani huyo lisema hayo jana wakati madiwani wakiwakilisha taarifa za maendeleo ya kata katika manispaa hiyo.


Alisema kuwa kwa muda mrefu barabara nyingi za kata hiyo zilikuwa hazipitiki jambo ambalo lilikuwa ni kero kubwa kwa wakazi wa kata hiyo. "Tunashukuru manispaa yetu kwa kutekeleza ilani ya CCM kwa kuhakikisha wamechonga barabara zote na sasa zinapitika," alisema.

Aidha diwani huyo alisema kuwa kata hiyo bado wanakabiliwa na changamoto ya ufinyu wa bajeti wa fedha za kuwezesha kamati za Ukimwi. Alisema kuwa kama kata walifanya jitihada za kuhakikisha wanadhibiti Ukimwi kwa kutoa elimu kwa vijana jambo ambalo limeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa.

Kwa upande wake Meya wa Manispaa ya Morogoro, Amiri Nondo alisema kuwa suala la kuchonga barabara ni mpango wa manispaa hiyo kwa kata zote ili kuhakikisha wananchi wanaondokana na kero hizo.

Alisema kuwa mpango wa awali ulikuwa ni kutengeneza barabara kwa kiwango cha lami hususani za mjini zote na kwamba kwa kiasi kikubwa umefanikiwa.

Hata hivyo meya huyo alisema kuwa mpango huo uende sambamba na utunzaji wa mazingira na kwamba sheria ya kutoza faini wanaochafua mazingira itiliwe mkazo zaidi bila huruma.

No comments:

Post a Comment