Na Said Hauni, Lindi
MAHAKAMA ya Mwanzo Mtama iliyopo Mkoa wa Lindi imemhukumu
mkazi wa mtaa wa Shekhe Badi,katika Halmashauri ya Manispaa ya Lindi,Said
Abdallah (21) kifungo cha mwaka mmoja gerezani, baada ya kupatikana na kosa la
kumtapeli mganga wa Jadi
. Hukumu hiyo ilitolewa hivi karibuni na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa
mahakama hiyo,Hamisi Katumba baada kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande
wa mashtaka.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo,Hakimu alimuuliza mshtakiwa kama
ana sababu za msingi ili mahakama hiyo,isimpe adhabu kali ambapo aliomba
asamehewe,kwani ni mkosaji wa mara ya kwanza na kwamba alilazimika kufanya
hivyo kutokana na hali ngumu ya maisha inayomkabili.
Hakimu Katumba akitoa hukumu katika kesi hiyo,alisema hakubaliani
na utetezi huo,kwani kazi si ya kuajiriwa pekee,kwani ardhi ipo angeweza
kuitumia kwa kazi ya uzalishaji mali mashambani,hivyo akamhukumu kifungo cha
mwaka mmoja gerezani ili iwe fundisho kwa wengine.
Awali, ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, Julai 21 mwaka huu,kati ya
saa 5 na 6 mchana,huko katika Kijiji cha Kilimahewa,Lindi vijijini mshtakiwa
akiwa na wenzake watatu,walifika nyumbani kwa mlalamikaji Hadija Bakari Mtondo
na kumtapeli kwa kumchukulia shahada ya kupigia kura na fedha taslimu sh.
30,000.
Imeelezwa pia kuwa fedha na shahada hiyo aliichukua kwa
madai ya kumtengenezea kitambulisho kinachomtambulisha kazi yake ya uganga wa
kienyeji anaoufanya. Mlalamikaji Hadija Bakari Mtondo akizungumza na gazeti
hili nje ya mahakama hiyo, alisema amefarijika na hukumu iliyotolewa dhidi ya
mshtakiwa wake, licha kukosa shahada na fedha zake.
No comments:
Post a Comment