12 August 2013

TEKNOLOJIA YA PANYA ITUMIKE KUKAGUA DAWA ZA KULEVYA



Goodluck Hongo
PANYA ni aina ya mnyama ambaye kitaalamu yupo katika kundi la wanyama wanaonyonyesha (mamalia) ambao wanapatika katika sehemu zote za nchi yetu.Tume z o e a k u o n a ama kusikia kuwa wanyama ambao wanatumika sana ni mbwa, farasi, ngamia na punda ambapo sehemu nyingi duniani wanyama hawa hutumika katika njia mbalimbali ikiwemo kubeba mizigo, kubeba watu, kuvuta toroli na wengine hutumika katika kuwafichua wahalifu kama wabeba unga ama mabomu.

Lakini kama ilivyo kwa wanyama ama ndege wanaofugwa panya nao huwa na maisha yao ya kila siku licha ya kuwa waharibifu wa mazao na wakati mwingine kutafuna hata nguo na kuuliwa kwa njia mbalimbali na hasa kwa kuwekewa sumu.Hali ni tofauti katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine Mkoani Morogoro (SUA) ambacho huwatumia panya katika kupima ugonjwa wa kifua kikuu na wakati mwingine panya hutumika katika kufichua mabomu yaliyotegwa ardhini katika baadhi ya nchi ambazo zilikumbwa na vita kubwa ikiwemo Angola na Msumbiji.
Mkufunzi Mkuu wa panya hao kutoka SUA Bw.Peter Luanda anasema panya hao ndio wanaotoa majibu ya uhakika katika upimaji wa kifua kikuu kuliko ambavyo binadamu anapima kwa kutumia darubini.Anasema mradi huo unajulikana kama APOPO ambapo huwafundisha panya hao kwa teknolojia mbili ambapo moja ni kwa ajili ya kugundua mabomu ya ardhini na nyingine ni kwa ajili ya kupima na kugundua kifua kikuu (TB) kwa kutumia makohozi ya binadamu.
Panya wanaotumika katika mafunzo hayo ni panya wa porini (panya buku) ambapo kitaalam wanaitwa ‘African giant potched rat’ ambapo kisayansi wanaitwa ‘cricetomys gambianus’ ambao huwakamata porini na kisha kuwapa mafunzo na wakati mwingine huwazalisha kutokana na mahitaji.
Panya huweza kuishi miaka nane hadi 10 ambapo panya mmoja huzaa watoto wanne hadi sita na hushika mimba kwa mwezi mmoja.
Mkufunzi huyo anasema panya hao huanza na mafunzo ya wiki mbili ambayo huyaita mafunzo ya mahusiano kati ya binadamu na panya na baadaye huwafundisha mlio unaoambatana na chakula ambapo kila panya anaposikia mlio huo hukimbilia eneo husika na akifika hapo hunusa matundu kuanzia matatu ambayo yamewekwa mahususi kwa ajili panya hao.
Matundu hayo huwekwa ili kumfundisha panya ambapo kati ya matundu matatu, tundu moja huwa linakuwa na chakula na hapo huanza kusikia mlio huo na kisha huzoea.
Hivyo kila mlio huo unapolia basi panya huamini kuwa muda wake wa chakula umefika hivyo akisikia tu mlio huo hukimbilia eneo lenye matundu na kuanza kunusa kila tundu na kisha kupata moja lenye chakula na huo ndio mtindo wa kuwalisha panya hao.
Baada ya kuzoea mafunzo hayo ndipo wanapohamisha chakula na kuweka makohozi yenye vimelea vyenye ugonjwa wa kifua kikuu (TB) ambapo jumla ya mafunzo hayo yote huchukua miezi minne hadi kukamilika kwake ambapo baada ya panya kuhitimu hupewa mtihani wa kumpima kama kweli anaweza kugundua makohozi yenye vimelea vya ugonjwa.
Anasema panya hao huwekewa sampuli 30 na kati ya hizo panya aliyehitimu anatakiwa apate 8/8 kati ya 22 ambazo hazina vimelea ambapo huwekewa matundu matatu na baadaye kuongezewe matundu hadi 10 na zoezi hilo huchukua wiki tatu hadi mwezi mmoja.
Anasema hiyo ni teknolojia rahisi na ya haraka ambayo haihitaji umeme na inakuwa na uhakika mkubwa kuliko teknolojia nyingine ambazo zinahitaji umeme ili zitoe majibu ambapo panya anaweza kugundua hata ugonjwa wa kifua kikuu ambao unaanza sasa.
Panya buku huwa hawana magonjwa na ugonjwa wao mkubwa wa panya buku ni kansa ambayo huipata katika masikio yao na mkiani ambapo tafiti zinaonesha kuwa kansa hiyo ya panya haiwezi kuambukiza.
Upimaji
Katika suala zima la upimaji hupitia hatua zaidi ya sita ambapo hatua ya kwanza ni kuchukua sampuli ya makohozi ya mgonjwa ambayo yamepimwa na kugundulika kuwa na ugonjwa huo na kisha APOPO huchukua ambapo hatua ya pili ni kuchemsha (inactiveted) ili kupunguza maambukizo ya ugonjwa huo kwa panya na wakufunzi (trainers) wanaopima hasa panya ambao hutumia kunusa na kugundua.
Hatua inayofuata ndio ya upimaji ambapo baada ya kupima inayofuata ndio panya anagundua sampuli ambazo awali zilipimwa maabara lakini panya anagundua kuwa katika sampuli hizo nyingine zina vimelea vya ugonjwa wa kifua kikuu licha ya kupimwa na darubini.
Baada ya APOPO kubaini wagonjwa wapya hurudisha majibu katika hospitali ambazo walichukua sampuli hizo ili kuzipima ambapo hospitali huwaita wagonjwa na kisha kuwapa taarifa na kuwaanzishia taratibu za kutumia dawa ambapo ili kuthibitisha ugonjwa huo APOPO hutumia panya wawili waliofuzu mafunzo vizuri ndio hutumika kupima.
Takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2012 panya waliweza kugundua wagonjwa zaidi ya 30,000 huku panya hao wakionesha wagonjwa wapya ambao walipimwa maabara lakini walionekana hawana ugonjwa wa kifua kikuu zaidi ya 2900 huku jiji la Dar es Salaam lilipima wagonjwa 10,000 na panya waligundua wagonjwa wapya zaidi ya 400.
Panya mmoja anaweza kupima wagonjwa 40 kwa dakika saba tu tofauti na mtu wa maabara ambaye anapima wagonjwa 25 kwa siku.
Mradi huo wa APOPO unafanyakazi katika hospitali 17 nchini ambapo zipo katika Mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro huku mradi huo ukitegemea zaidi fedha za wafadhili.
Mabomu
Mbali na hilo panya hao pia hufundishwa jinsi ya kukagua ama kufichua mabomu yaliyoko ardhini ambapo mafunzo yao ni kama ya kugundua ugonjwa wa kifua kikuu ila kinachotofautisha mafunzo hayo ni hufundishwa hasa kuelekea ardhini.
Katika mafunzo hayo panya huwekewa kitu mfano wa yai (tea eggs) ambavyo hufukiwa ardhini na panya hufanya kazi ya kufukua na akigundua basi huongezewa urefu zaidi kwenda chini ya ardhi.
Hatua inayofuata ni panya kuwekwa eneo lenye ukubwa wa mita tano na hapo akishinda vizuri huongezewa ukubwa wa eneo hadi kufikia mita 20 (advanced stage) ambapo baada ya kufanikiwa zoezi hilo hapo ndipo hupewa mtihani ili kuthibitisha kama kweli anaweza kugundua mabomu hayo.
Mafunzo ya panya kugundua mabomu yaliyotegwa ardhini huchukua mwezi mmoja na nusu hadi miezi miwili na ndipo wanapopewa mitihani.
Mafanikio
Mafanikio makubwa ya kuwafundisha panya hao ni kupunguza zoezi la upimaji ambalo linafanyika kwa haraka zaidi kuliko kutumia darubini ambapo mbali na hilo majibu ya wagonjwa wapya yatapatikana haraka kisha kuanza kutumia dawa na kusaidia zaidi kupunguza maambukizi mapya ya ugonjwa wa kifua kikuu.
“Ni teknolojia rahisi na ni ya awamu ya pili baada ya kutumia darubini ambapo panya wanagundua wagonjwa 15 hadi 18 kwa wiki ambapo darubini imeshindwa kuwatambua baada ya kupima sampuli hizo,” anasema Bw. Luanda
Bwana Luanda anasema kuwa kutokana na mazoea na binadamu kwa muda mrefu na mfumo mzima wa kulishwa kupitia mlio maalumu panya hao hata ukiwaachia hawawezi kukimbia popote na unaweza kumkamata bila tatizo.
Mafaniko ya panya hao yameonekana zaidi nchini Msumbiji ambapo wamefanikiwa kusafisha kwa kugundua mabomu yaliyokuwa ardhini katika majimbo ya Manika, gaza ambapo wamesafisha eneo kubwa na kwa sasa wapo katika majimbo mengine wakiendelea na kazi hiyo ya kugundua mabomu.
Panya hao pia wamefanikiwa kugundua mabomu zaidi ya 470 yaliyokuwa ardhini ambapo 424 ni mabomu yanayohusiana na watu na tisa yalikuwa ya kulipulia magari na vifaru.
Mbali na hilo lakini pia wamegundua mabomu makubwa kabisa 43 ambayo yanauwezo wa kulipua eneo kubwa huku mabaki ya silaha yaliyogunduliwa na panya hao ni zaidi ya 800.
K w a s a s a p a n y a h a o wanafanyakazi ya kugundua mabomu katika nchi mbalimbali duniani ikiwemo Msumbiji, Angola, Thailand, Cambodia ambao wote ni kutoka SUA na kupelekwa katika nchi hizo kwa ajili ya kufanya kazi ya kugundua mabomu hayo ya ardhini huku nchi zingine zikiomba kupelekewa panya hao ili wawatumie katika kugundua mabomu hayo.
Changamoto
Changamoto kubwa inayoukabili mradi huo ni kutegemea fedha za wafadhili tu ambapo hiyo ndio sababu kubwa ya mradi huo kushindwa kufika katika hospitali zingine zilizoko hapa nchini huku Serikali ikiwa haifadhili mradi huo.
Kwa hali hii ni vyema Serikali ikaongeza wataalamu wanaoweza kuwatunza panya hao kama ambavyo jeshi la polisi linavyowatunza mbwa kwa ajili kufanya kazi maalumu ikiwemo kugundua dawa za kulevya na mabomu.
Hii ni teknolojia ambayo ni rahisi ni vyema Serikali na wadau wengine wa masuala ya afya wajitokeze ili kuunga mkono juhudi za SUA katika kutokomeza ugonjwa wa kifua kikuu ambapo bado ni tishio katika nchi hii pamoja na uuzaji dawa za kulevya.

No comments:

Post a Comment