HOTUBA ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete ya
mwisho wa mwezi Julai inaendelea kujadiliwa na watu katika maeneo yote kwa
kadri ya upeo wanavyoiona.Hoja hii ya uchokozi wa Rais Paul
Kagame wa Rwanda,
kimtazamo inategemewa kujadiliwa na kutafakari kwa kina. Tabia aliyoionyesha Rais Kagame kwa
upande wangu imenikasirisha kwa sababu kauli zake na za Serikali yake
inachochea uvunjifu wa amani na utulivu katika nchi za Maziwa Makuu
Inaaminika Rais Kagame ndiye Amiri
Jeshi Mkuu wa wapiganaji wa kundi la M23.
Hili la kuichokoza Tanzania, ni
sawa na volcano inayotikisa chini kwa chini na inaweza kulipuka wakati wowote.Matusi, kejeli anazofanya Rais Kagame,
sio za bahati mbaya, anajua anafanya nini na wala si kwamba hakujua maana ya
ushauri wa Rais Kikwete.
Inavyoonekana akiwa Amiri Jeshi wa
majeshi ya M23 anayowasaidia, amechukizwa na hatua ya Tanzania ya
kupeleka askari kulinda amani huko mashariki ya Kongo.Tabia anayoonyesha Rais Kagame
haipishani sana na ile ya marehemu Dikteta Idd
Amini Dada wa Uganda.
Bila shaka Rais Kagame ana ulevi wa madaraka na hii jeuri na kiburi
anachoendelea nacho hajui athari zake.
Rais Kagame inaonekana kuwa ni mwenye
tamaa na mbinafsi na hana ari ya kujenga umoja wa Afrika na kama
atakuwa na ari hiyo atakuwa amepotea.
Hana hata mkakati wa kutufikisha ama
tufikie lengo hilo lililoasisiwa miaka mingi
iliyopita na wazee wetu wa Afrika kama vile
Julius Nyerere, Patrice Lumumba, Sekouw Toure, Ahmed Benbela, Tafawa Balewa nk.
Wakati Kagame anafanya upuuzi huu
tumebakiza siku chache kusherehekea siku ya amani duniani. Nchi za Afrika
zikiwa sehemu ya jumuia pana duniani, tutaungana na Mataifa mengine Septemba 21
kuadhimisha siku hiyo.
Na hili ni azimio linalotokana na wakuu
wa Serikali za nchi wanachama wa Umoja wa Afrika uliotolewa Tripoli nchini Libya Agosti 31, 2009,
iliyoenda sambamba na kauli mbiu ya “Make peace happen” yaani fanya amani
iwepo. Lengo lilikuwa ni kudumisha amani.
Mwenzetu Kagame hayataki hayo, anataka
“fanye vita itokee” “let the war happen” sisi tunamshangaa. Sijui kama Kagame
amesahau yaliyotokea nchini mwake. Matokeo ya vita na mamilioni ya watu wasio
na hatia kupoteza maisha yao, kujeruhiwa hususan
watoto na wanawake wajawazito ambao wanataabika sana.
Vita inaharibu miundombinu ambayo
Serikali zetu imejitahidi kuzijenga kwa fedha nyingi na hata kwa mikopo toka
nje. Vita inavuruga sana
uchumi na maendeleo ya nchi. Fedha zote zilizokuwa zielekezwe kwenye huduma
muhimu za jamii kama afya, elimu, maji nk.
Baadala yake zinaelekezwa kwenye ununuaji wa silaha.
Na kwa sababu Kagame hajui kwamba
tutakakaonunua silaha hizo ni kwa hao hao waliomsukuma atuchokoze yeye
anawasikiliza. Rais Kagame atambue kwamba moja ya mbinu na silaha kubwa
inayotumika na wakubwa hao ni kutugawa ili Afrika idhoofike isiwe na nguvu.
Lengo lao ni kutafuta fursa ili
kuzifikia rasilimali kwa ajili ya kujiimarisha kiuchumi. Rasilimali zetu,
zikiwemo ardhi, gesi, mafuta, uranium ni bidhaa adimu sana
duniani lakini Rais Kagame halielewi hilo.
Kwa taaluma yake ya kijeshi, Rais
Jakaya Mrisho Kikwete ametufungua masikio Watanzania kwamba, siri ya vita siku
zote ni kutomdharau adui. Kwa maana nyingine ameturudisha kwenye maandiko
matakatifu ya Biblia juu ya vita ya Goliathi na Daudi.
Goliath lilikuwa jitu kubwa lenye
miraba minne, lakini lilibwagwa na mtu mdogo Daudi. Udogo wa nchi ya Rwanda
tusiudharau hatufahamu Rais Kagame anafanya jeuri hiyo kwa maandalizi yapi.
Vita ni kuwahi ndio sababu katika
hotuba yake Rais Kikwete alisema “Amesikia mengi sana
yanayozungumzwa na kudaiwa kupangwa na kufanywa na Serikali ya Rwanda dhidi yake yeye mwenyewe na nchi ya Tanzania. Kwa
hiyo kamwe hawezi kuyapuuza ingawa hapendi kuyaamini moja kwa moja”
Hii maana yake nini? Maana yake ni
kwamba tuwe na hadhari. Anatukumbusha yale ya Nduli Idd Amini, naye alianzisha
chokochoko zinazofanana sawa na hizi za Kagame, hivyo inawezekana kukawa na
ukweli wa kauli za Kagame.
Kuna haja ya kuchukua hatua za dharura
na haraka za kuilinda nchi yetu. Hili sio suala la hiari, ni jambo la lazima
ili kuja kuhimili uvamizi wowote endapo utatokea.
Labda nitoe ushauri kwa Serikali yetu
kwamba, ianze kuandaa mazingira ya kiulinzi yatakayotokana na uvamizi wowote,
kwani “HATUIJUI SIKU HATA SAA.” Turejeshe kwa haraka na kwa msisitizo mafunzo
ya mgambo. Liwe ni suala la kufa na kupona, lifanywe na kupangwa kimkakati na
kwa malengo.
Ikumbukwe kwamba, vijana wale
waliohitimu mgambo miaka ya 1970 ndio baadaye lilikuja kuwa jeshi la akiba na
ndilo tulilitumia katika vita ile dhidi ya Idd Amini. Vijana wale wamekuwa watu
wazima sasa na wengine walijiunga na Jeshi la Wananchi wa Tanzania.
Kwa sasa tuna upungufu mkubwa wa jeshi
la akiba, kwani baada ya vita ile tumezembea katika mafunzo ya mgambo. Vijana
karibu wote waliopo leo hawajapitia jeshi.
Tuwaandae vijana sasa ili waanze
kujenga uzalendo miongoni mwao, kuvunja matabaka ya itikadi za kisiasa
zilizowagawa ili wabaki kitu kimoja, nia ni kuilinda Tanzania
kama mboni ya jicho. Kila Mtanzania mahali
alipo aanze kujitayarisha ili kujitoa mhanga endapo litatokea lolote.
Serikali nayo kwa upande wake iangalie
matumizi yasiyo ya lazima yanayohitaji fedha za kigeni. Tuwe na akiba ya
kutosha.
Tanzania
ni nchi inayosifika kuwa na amani, utulivu, demokrasia, utawala bora na haki za
kibinadamu. Tanzania na Rwanda zina
uhusiano wa undugu, na umeenda mbali zaidi, kuwa na uhusiano wa diplomasia ya
uchumi kwani wote tuko katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na (SADC) nchi ya
Kusini mwa Afrika, kwa hiyo matokeo yoyote ya vita sote sisi tutakuwa
tumeathirika na jumuiya hizo nazo zitaathirika.
Hata hivyo Rais Kagame anapaswa kuelewa
kuwa mapenzi kwa nchi ya Rwanda
yatapungua, lakini undugu wetu hautaisha.
Vilevile masuala haya hayataki ubabe
wala jazba bali ayaangalie kwa uzito kuhusiana na hoja za Rais Kikwete, kwa
manufaa ya nchi zetu na za maziwa makuu, sio leo tu bali kwa muda mrefu.
Rais Kagame alitoa lugha zisizostahili
dhidi ya Rais Kikwete katika sherehe ya kuhitimu mafunzo ya kijeshi ya maofisa
45 wa jeshi lake Julai mwaka huu, ambapo alisema ushauri
wa kufanya mazungumzo na waasi wa FDLR ni ujinga na haupo katika historia ya
Wanyarwanda.
“Nilinyamaza kimya kwa sababu sikupenda
kusikiliza ushauri kuhusu FDLR, kwa sababu nafikiri ni upuuzi ulioambatana na
ujinga. Hatuwezi kuacha maisha yetu kama
Wanyarwanda tunavyoishi sasa. Ushauri wa Kikwete ni sawa na kucheza na makaburi
ya watu wengi ambao ni ndugu zetu,” alisema Kagame.
Katika hotuba ya Rais Kikwete alisema
uhusiano wa Tanzania na Rwanda unapitia katika wakati mgumu na mtikisiko, baada
ya yeye kutoa ushauri kwa Serikali ya Rwanda kuzungumza na mahasimu wao na
kwamba hilo linadhihirika katika kauli zinazotolewa na viongozi wa Rwanda.
“Napenda kuwahakikishia Watanzania
wenzangu na ndugu zetu wa Rwanda kuwa mimi, Serikali ninayoiongoza na wananchi
wa Tanzania, tunapenda kuwa na uhusiano mzuri na ushirikiano wa karibu na
Rwanda kama ilivyo kwa nchi zote jirani,” alisema Rais Kikwete.
Alisema nchi hizo ni jirani na kila
moja inamuhitaji mwenzake, hivyo lazima ziwe na uhusiano mwema na ushirikiano
mzuri.
“Nasisitiza kuwa mimi na Serikali
ninayoiongoza tutakuwa wa mwisho kufanya kitendo au vitendo vibaya dhidi ya Rwanda au nchi
yoyote jirani au yoyote duniani. Hatuna sababu ya kufanya hivyo, kwani ni mambo
ambayo hayana tija wala masilahi kwetu,” alisema.
Alisema nchi hizo mbili zimekuwa zikijihusisha
na mambo ya kukuza na kujenga ujirani mwema, kusisitiza kwamba hiyo ni moja ya
nguzo kuu ya Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania
No comments:
Post a Comment