16 August 2013

IAAF YAFUATA NYAYO ZA FIFA Na Amina Athumani
SHIRIKISHO la Kimataifa la Riadha (IAAF), limezitaka serikali kuacha kuingilia masuala ya mchezo huo na kuachia vyama husika kuisimamia na wao wakibaki kama wadhamini.Hatua kama hiyo pia hutumiwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), ambalo halitaki wanachama wake kuingiliwa na serikali.

Rai hiyo imetolewa katika Mkutano Mkuu wa marais wa mchezo huo Duniani uliofanyika Moscow, Urusi kabla ya kuanza kutimua vumbi mashindano ya Dunia, ambayo yanaendelea nchini humo na kuhudhuriwa na washiriki 206.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Rais wa Chama cha Riadha Tanzania (RT) Antony Mtaka, alisema mkutano huo ulijadili masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na hilo ikiwa ni kwa manufaa ya mchezo wa raidha kwa kila nchi.
Alisema pia kulijadiliwa utumiaji wa dawa za kuongeza nguvu, ambazo zimekuwa ni gumzo katika maendelo ya michezo, ambapo wanariadha wengi wamekuwa wakibainika kutumia dawa za kuongeza nguvu na kuweza kushinda katika mshindano mbalimbali.
Rais huyo alisema, kutokana na maagizo hayo, RT imejipanga kusimamia kila nyanja kuhakikisha mchezo huo unasimamiwa ipasavyo.
Mtaka alielezea mikakati mbalimbali waliyoiweka katika kuhakikisha mchezo huo unapiga hatua kubwa hapa nchini ikiwa ni pamoja na kuandaa katiba ya RT, itakayobeba mambo ya msingi ya chama hicho.
Alisema pia hawakusita kuomba msaada wa kuletewa walimu wa kimataifa, watakaoweza kuwafunza wachezaji wa hapa nyumbani na katika barua yao wamemuomba, Rais Jakaya Kikwete kuwaletea makocha kutoka Jamaica wakiamini wana uwezo mkubwa wa kufundisha wanariadha.
Rais huyo alisema mikakati iliyopo sasa ni kuhakikisha wanaendeleza vipaji vya riadha vilivyovumbuliwa katika mashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA, hususani vijana waliopata nafasi ya kushiriki mashindano ya Afrika Mashariki.
Alisema ipo mipango mizuri ya kuhakikisha vijana hao, wanapatiwa mafunzo katika vituo vya michezo na tayari wameshaomba kupunguziwa ada ya kupeleka vijana katika kituo cha michezo, kilichopo nchini Kenya.

No comments:

Post a Comment