Na Mashaka Mhando, Korogwe
CHAMA Cha Wananchi (CUF) wilayani Korogwe kimetamba kushinda
ubunge katika jimbo la Korogwe Mjini, kutokana na madai kwamba mbunge aliyepo
sasa, Yusuph Nassir kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), kushindwa kukidhi
matarajio ya wananchi wa jimbo hilo tangu achaguliwe mwaka 2010
. Akizungumza na waandishi wa habari mjini humo, Kaimu Katibu wa CUF
wilaya ya Korogwe, Ibrahim Abdillahi alisema kuwa kitendo cha mbunge huyo
kulikimbia jimbo lake kwa kipindi kirefu tangu achaguliwe kinawapa nafasi ya
kujinadi kwa wananchi kisha kushinda kirahisi mwaka 2015 kwa kuwa wananchi wa
jimbo hilo, wana kiu kubwa ya maendeleo hasa kasi aliyokuwa nayo Mkuu wa wilaya
hiyo, Mrisho Gambo.
"Wananchi wa Korogwe mjini hatuna wa kutusemea sio bungeni
wala kwenye mikutano ya hadhara ya viongozi wa Serikali wanapokuja Korogwe,
mbunge wetu hatujui nini kimempata kwa sasa...Haonekani kwenye mikutano yake
hata ile ya viongozi wa kiserikali wanaokuja kutembelea jimbo lake,"
alisema Ibrahim.
Alisema mbunge huyo tangu amechaguliwa kuwa mbunge mwaka 2010
alipomwangusha, Joel Bendera (sasa Mkuu wa Mkoa Morogoro), hajawahi kufanya
mkutano wowote na wananchi wa jimbo lake hatua ambayo kisiasa wanaielezea kama
kukosa dira na mwelekeo wa kugombea tena katika kipindi kijacho kwa kuwa
atakosa la kuwaeleza wananchi na wakamkubalia.
Akitoa sababu za kueleza suala hilo Ibrahim ambaye pia aliwahi
kuwa Mkurugenzi wa Haki za Binadamu wilayani hapa kupitia chama hicho, alisema
kuwa hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Tanga Luteni (mstaafu) Chiku Gallawa alifanya
ziara wilayani hapo lakini mbunge huyo hakuwepo wala kushiriki ziara yake hatua
ambayo wananchi wanashindwa kuelewa ni nini kimempata.
Alisema hivi karibuni halmashauri ya mji ilitenga viwanja
takribani 2000 na kuviuza kati ya kiasi cha shilingi milioni 1.8 hadi shilingi
milioni 5, lakini wananchi wa jimbo hilo hawakuwa na sehemu ya kupeleka
malalamiko kwa vile kiasi hicho ni kikubwa na kwamba wenye uwezo wa kununua ni
wageni tu na wananchi wa Korogwe hawawezi kiasi hicho.
Ibrahim alisema endapo wangekuwa na mbunge angeweza kuwatetea
kuonesha kwamba wananchi wa mji wa Korogwe hawana kipato kinachoweza kuwafanya
waweze kununua kiwanja cha bei hiyo hivyo, ilikuwa ni sehemu nzuri kwa
mwakilishi wao kujenga hoja na kuwatetea wananchi wake.
Hata hivyo akizungumza na mwandishi wa habari kuhusiana na madai
hayo, Mbunge huyo alisema kuwa malalamiko yanayotolewa dhidi yake hayana ukweli
wowote bali yana lengo la kumchonganisha na wananchi huku akidai kukosekana
kwake kwenye ziara ya Mkuu wa Mkoa inatokana na kuhudhuria katika mkutano wa
wabunge Jumuiya ya Madola uliofanyika kwa siku 10 tangu Julai 13 hadi 27,
nchini Namibia.
"Kwanza huyo Ibrahim ni ndugu yangu ninamwelewa vizuri hao
watu wa CUF hawamjui historia yake hadi wakampa huo ukatibu wa wilaya na hawatashinda
wakiwa na katibu huyo...na suala la kutokuwepo kwenye ziara ya RC mimi
niliongoza ujumbe wa mkutano wa Jumuiya ya Madola tulikuwa Namibia kwa siku
10," alisema Nassir.
Kuhusu suala la viwanja alisema bei iliyopangwa na
Halmashauri ya Mji ni rahisi kiasi kwamba mwananchi yeyote anaweza kununua na
kumiliki kiwanja tofauti na maeneo mengine ya nchi wanavyouza ambayo ni bei
kubwa kiasi cha wananchi kushindwa lakini hata hivyo alisema endapo mkazi wa
Korogwe anataka kiwanja katika eneo la mji anaweza kwenda Kwamsisi na atanunua
kiwanja kwa bei ya sh. 200,000.
No comments:
Post a Comment