02 August 2013

CHAMA CHA MUGABE CHAJITANGAZIA USHINDIHARARE, Zimbabwe
CHAMA cha Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, ZANU-PF, kimedai jana kupata ushindi wa kishindo, ambao utamfanya kuendelea kuwa madarakani kwa miaka mingine mitano.Rais Mugabe ni kiongozi aliyekaa madarakani kwa muda mrefu kuliko kiongozi mwingine yoyote Afrika, lakini chama kikuu cha upinzani kimedai kulikuwa na “udanganyifu mkubwa” wa kura
. Uchaguzi uliofanyika juzi ulikuwa wa amani katika taifa hilo la kusini mwa Afrika, lakini madai ya kutatanisha yametangaza mgogoro mkali juu ya matokea ambayo yanaongeza nafasi ya kurudiwa ghasia za uchaguzi wa 2008.Kutoa mapema matokea yasiyo rasmi nchini Zimbabwe ni kosa kisheria na polisi wamesema watamkamata yoyote atakayefanya hivyo. Mamlaka ya Uchaguzi wanatarajia kutangaza matokeo rasmi Agosti 5.
 Lakini chanzo cha habari mwandamizi katika chama cha ZANU-PF cha Rais Mugabe mwenye umri wa miaka 89, ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema matokeo tayari yako wazi.“Tumeuchukua uchaguzi huu. Tumekizika MDC. Hatukuwa na shaka yoyote, kwani tulijua tutashinda,” chanzo hicho kililiambia shirika la habari la ‘Reuters’ la Uingereza kwa simu.
Akijibu madai hayo, chanzo cha ngazi ya juu katika chama cha MDC cha Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai aliuelezea uchaguzi huo kama wa “udanganyifu mkubwa”.“Wazimbabwe wamedanganywa na ZANU-PF na Mugabe. Hatuwezi kukubali,” chanzo hicho kilichokataa kutajwa jina lake, kiliiambia ‘Reuters.’
Kwa mujibu wa Reuters, MDC ilitarajiwa kufanya mkutano wa dharura jana jioni.
Huku askari wa ghasia wakichukua nafasi katika makao makuu ya MDC katikati ya Harare, mwangalizi binafsi wa uchaguzi huo, ambaye pia hakuweza kutajwa kwa kuogopa kukamatwa alisema matokeo ya awali yalikuwa yakionekana kama “balaa” kwa Tsvangirai.
Waangalizi kutoka magharibi walizuiliwa, lakini mkuu wa mpango wa uangalizi wa Umoja wa Afrika alisema juzi uchaguzi huo awali ulionekana wa “amani, umepangwa vizuri na wa huru na haki” - tathmini inayopingwa na MDC pamoja na mashirika ya habari binafsi.

No comments:

Post a Comment