27 August 2013

CCM YAMTIMUA UWAKILISHI MANSOUR

  • HALMASHAURI KUU YARIDHIA,YATEUA MAKATIBU


Na Pendo Mtibuche, Dodoma
HALMASHAURI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), jana imemaliza kikao chake cha siku tatu
mjini Dodoma chini ya Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete. Kikao hicho kimeridhia baadhi ya mapendekezo ya Kamati Kuu ya CCM, pamoja na kumvua uanachama Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Kiembesamaki, Jimbo la Mjini Magharibi, Zanzibar, Bw. Mansour Yusuf Himid.

 Bw. Himid ni kada wa siku nyingi katika visiwa vya Zanzibar na Waziri wa zamani, aliibua mjadala ndani ya CCM akitaka Zanzibar pate haki ya kuwa na mamlaka zaidi ya kujiamulia mambo yake ndani ya Muungano. Mwanasiasa huyo, ambaye amepata kuwa Mweka Hazina wa CCM Zanzibar wakati wote wa uongozi wa Rais Mstaafu, Amani Abeid Karume, amekuwa mtetezi mkubwa wa muundo wa Muungano wa Serikali tatu badala ya ule wa Serikali mbili.
Halmashauri Kuu ilitarajiwa kutoa uamuzi wa ama kufukuzwa au kumbakiza kundini baada ya uongozi wa ngazi ya Mkoa, Wilaya pamoja na Kamati Maalumu ya CCM Zanzibar, kupendekeza atimuliwe kutokana na msimamo huo. Taarifa iliyotolewa na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Bw. Nape Nnauye, alisema baadhi ya tuhuma zilizokuwa zikimkabili Bw. Himid ni kushindwa kusimamia malengo ya chama na kutekelezamasharti ya uanachama.Kushindwa kutekeleza wajibu wa mwanachama na kukiuka maadili ya kiongozi wa CCM pamoja na kuikana Ilani ya chama ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010-2015 na kuisaliti CCM. "Kwa uamuzi uliofikiwa wa kumvua Bw. Himid uanachama wa CCM, kwa sasa si kiongozi tena wa CCM," alisema. 
Hata hivyo, Halmashauri Kuu ya CCM ilijadili kwa kina muundo wa Muungano na suala la Bw. Himid ambaye alishatangaza kuwa, yuko tayari kufukuzwa kwa sababu ya kutofautiana na chama chake juu
ya muundo wa sasa wa Muungano. Pia kikao hicho kimeridhia uteuzi wa Makatibu wateule wapya wa jumuiya za CCM, Umoja wa Vijana (UVCCM), Jumuiya ya Wazazi na Umoja wa Wanawake Tanzania
(UWT).Mapendekezo ya Kamati Kuu ambayo yameridhiwa na NEC, Sixtus Mapunda ameteuliwa kuwa
Katibu wa Umoja wa Vijana CCM, ambaye awali alikuwa Kaimu Katibu wa CCM mkoani Morogoro.
Bw. Seif Shabani Mohamed, ambaye ni Mjumbe wa NEC kutoka Pemba aliteuliwa nafasi
ya Katibu wa Jumuiya ya Wazazi ambapo Katibu wa UWT ni Amina Makilagi ambaye ameendelea
kushika wadhifa huo. Mapunda atachukua nafasi iliyokuwa imeshikiwa na Martine Shigela ambaye ameongoza UVCCM kwa kipindi cha miaka mitano sasa ambapo Bw. Mohammed kutoka Pemba akichukua nafasi iliyokuwa kishikiliwa na Hamis Suleiman Dadi ambaye pia amekuwa katika wadhifa huo kwa miaka mitano.
Kikao hicho pia kimeridhia mapendekezo ya Kamati Kuu kwa ajili ya kuziba nafasi za Makatibu wa CCM mikoa mitatu ya Morogoro, Kaskazini Pemba na Geita. Mikoa hiyo ilikuwa haina Makatibu kwa muda mrefu kutokana na sababu mbalimbali. Walioteuliwa na mikoa yao kwenye mabano ni pamoja na Msaidizi Kitengo cha Uchaguzi CCM, Ofi si Ndogo Makao Makuu ya chama, Romuli Rojas John (Morogoro). Wengine ni aliyekuwa Katibu Wilaya ya Mkinga, Kassim Mabrouk Mbarak (Kaskazini  Pemba) na aliyekuwa Katibu wa CCM Igunga, Mary Maziku (Geita). Kuhusu sakata la madiwani wa Bukoba Mjini, mkoani Kagera, chama hicho kilisema suala hilo linaendelea kushughulikiwa na baada ya kikao cha NEC, Kamati Kuu itaendelea kukutana na viongozi wa Wilaya ya Bukoba, Mwenyekiti wa CCM na Katibu wa Wilaya hiyo. Mapema kabla ya kikao cha NEC, Kamati Kuu ilikutana na Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki, Meya wa Manispaa ya Bukoba Mjini Dkt. Anatory Amani na kuwahoji. 

No comments:

Post a Comment