Na Eckland Mwaffisi
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeipongeza
Serikali kwa kusikiliza kilio chao na kukubali kujadili namna ya kusitisha tozo
ya sh. 1,000 kila mwezi kwa kila laini ya simu iliyopaswa kulipwa na watumiaji
wa simu za mkononi.
Pongezi hizo zimetolewa
jana na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM, Bw. Nape Nnauye wakati
akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu akiwa mkoani Kigoma na kusisitiza
kuwa, chama hicho kiliitaka Serikali iangalie njia nyingine ya kupata vyanzo
vya mapato badala ya kodi hiyo.
Alisema, kwa
kuwa Serikali imeamua kulirudisha suala hilo bungeni, CCM inatoa wito kwa
wabunge ambao wengi wao wanatoka chama tawala, kulijadili suala hilo kwa makini
na kuishauri Serikali vyanzo vingine vya mapato.
“CCM ni chama
makini kinachowajali wananchi ndio maana tulianza kupiga kelele za kupinga tozo
hii ambayo ingewaumiza Watanzania...leo (jana) hii Waziri wa Fedha, William
Mgimwa ametangaza msimamo wa Serikali ambao umezingatia agizo alilotoa kiongozi
wa nchi Rais Jakaya Kikwete.
“Katika agizo lake, Rais Kikwete
ameitaka Wizara ya Fedha ikutane na wadau ili kuangalia namna nyingine ya
kupata vyanzo vya mapato badala ya kodi hii,” alisema Bw. Nnauye.
Hata hivyo juzi Waziri Mgimwa alisema
suala hilo litafikishwa bungeni mjini Dodoma Agosti mwaka huu na kumalizwa
kisheria baada ya Rais Kikwete kuitaka Wizara hiyo, Wizara ya Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia na kampuni za simu kumaliza utata uliojitokeza juu ya
kodi hiyo.
Awali Umoja wa Wamiliki wa Kampuni za
Simu nchini (MOAT), ulitoa maoni yao ukitaka kodi hiyo ifutwe baada ya
kulalamikiwa na wadau wa sekta ya mawasiliano.
Mbali ya MOAT, baadhi ya viongozi wa Serikali, wabunge na wananchi nao
walipinga kodi hiyo wakidai itaongeza ugumu wa maisha kwa watumiaji wa simu za
mkononi hasa wa kipato cha chini.
No comments:
Post a Comment