30 July 2013

YANGA WAGOMA MECHI ZAO KURUSHWA NA AZAM MEDIA



Na Elizabeth Mayemba
UONGOZI wa klabu ya Yanga umesema kuwa haupo tayari mechi zake za Ligi Kuu Tanzania zirushwe na Televisheni ya Azam kwa kuwa utaratibu uliotumika haukuwa mzuri na kuna kasoro nyingi.Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa klabu hiyo Yusuf Manji alisema hivi karibuni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) liliunda Kamati ya Ligi chini ya Bodi ya Mpito (TPL), ambayo ni msimamizi mpaka hapo bodi itakapochaguliwa kidemokrasia
."Bodi hii imeamua peke yake kuingia katika mkataba wa miaka mitatu na kampuni inayoitwa Azam Media, ambayo inamapromota wake wale wanaomiliki Azam FC, hivyo makubaliano ambayo Bodi ya TPL inatarajia kuingia na Azam Media, Kamati ya Utendaji ya Yanga tunapinga," alisema Manji.Alisema wanapinga kwa misingi ifuatayo:Kwamba bodi iliyopo sasa ya mpito ambayo ilitakiwa kutenguliwa na bodi iliyochaguliwa kidemokrasia kwa kupitia uchaguzi ujao, haitakiwi kuingia katika mikataba ya miaka mingi wakati inakaribia kuondoka katika ofisi.
Manji alisema pia Bodi ya TPL iliyopo hivi sasa haikuchaguliwa kidemokrasia na vile vile haina mjumbe hata mmoja aliyeteuliwa kutoka Yanga.Alisema kwa utaratibu wa dunia nzima haijawahi kutokea katika ligi ya soka ya kisasa kulazimishwa kwa klabu inayoshindana katika ligi kuachia kazi zake za urushwaji wa michezo zichukuliwe na chombo cha habari cha klabu pinzani. 
"Mfumo (undertaking) ambao TPL inataka kuanzisha kwa njia ya kulazimisha mkataba kwa Yanga iachie urushwaji wa michezo yake ya soka irushwe na Azam TV, unatishia sana uwepo wa msingi wa ushindani katika soka la Tanzania.
"Makubaliano kati ya TPL na Azam Media kuhusu utaratibu wa malipo yanasema kwamba klabu ya Yanga na klabu nyingine zitakazoshiriki katika ligi kuu watapata mgawo sawa wa mapato ya urushwaji wa michezo hii, ambayo Yanga inapinga kwa sababu kama inavyofanyika duniani kote kwenye ligi zilizofanikiwa angalau kutofautisha mgawanyo wa mapato kati ya timu kufuatana na matokeo ya mwisho wa ligi," alisema Manji.
Alisema Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo, sio kwamba tu haikubaliani na mgawanyo sawa wa mapato ambao hautofautishi kati ya timu ya kwanza katika ligi na timu ya mwisho, lakini pia ukosefu wa viwango vitakavyolipwa.Kwani kuna klabu zenye ufuasi wa mashabiki wengi, vinavyoendeshwa na wanachama na visivyopata ruzuku serikalini.
Aliongeza kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Mpito ya TPL ni Mkurugenzi mwandamizi wa makampuni ya Azam hivyo mazungumzo kati ya TPL na Azam ni ya mashaka.
Aliongeza kuwa Yanga na Azam FC wanauadui wa kimichezo na kutolea mfano wakati Mrisho Ngassa alipokuwa Azam FC baada ya kuona Yanga wanamtaka wakamkopesha kwa nguvu Simba.
Pia mkataba kati ya Azam Media na TPL haukushindanishwa na vyombo vingine vya habari, vile vile mkataba huo unaonesha kuwa MoU iliyokusudiwa kuwekewa saini na TPL haikufikishwa Yanga kwa ajili ya mapitio kisheria licha ya klabu hiyo kuomba hilo.
"Kwa mfano moja ya vyanzo muhimu vya mapato Yanga ni viingilio vya mlangoni vitokanavyo na michezo ya soka ambayo urushwaji wa michezo hii itapunguza mapato.
"Kwa wastani michezo ya Yanga kwa Dar es Salaam huingiza sh.milioni 50 kwa kila mchezo na ikishuka kidogo ni kwa asilimia 25 tu katika mahudhurio ya mechi za Yanga zinafikia mara mbili ya mapendekezo ya mapato takriban sh.milioni 8.3 kwa mwezi kupokelewa na Yanga kutoka mradi wa kibiashara kati ya TPL na Azam Media," alitolea mfano Manji.

No comments:

Post a Comment