29 March 2011

Serikali yamwaga misaada kwa Babu

*Yatamka dawa yake haina madhara kwa binadamu
*Barabara inayokwenda huko sasa kukarabatiwa
*Kituo cha afya Samunge kuboreshwe, maji yapelekwa

Mchungaji Mwasapile Kushoto na Kulia ni Waziri Mkuu M.Pinda

Na Waandishi Wetu

SERIKALI imeiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Ngororo mkoani Arusha kuhakikisha inaimarisha huduma kijijini Samunge kama moja ya
njia ya kusaidia maelfu ya wananchi wanaomiminika kupata tiba ya 'kikombe' kwa Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Ambilikile Mwasapile.

Pia imetangaza maeneo makuu matatu ambayo magari yote yanayokwenda Loliondo yatakusanyika kabla ya kuruhusiwa kuanza safari ya kwenda kwa Babu, huku Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ikiweka bayana kuwa dawa hiyo haina madhara kwa binadamu.

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari jijijini Dar es Salaam jana, Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda alipongeza hatua ya mchungaji huyo kusitisha kwa muda utoaji huduma ili kupunguza msongamano ulipo sasa eneo hilo.

Akijibu swali lililotaka kujua msimamo wa serikali kuhusu kusadia tiba inayotolewa na Mzee Mwasapile maarufu kama 'Babu,' Bw. Pinda alisema kutokana na hali ilivyo, kuna kila sababu eneo hilo kuangaliwa vizuri wakati huu ambapo maelfu ya watu wanamiminika kupata tiba.

Alisema serikali imekubali ombi la mchungaji huyo kutaka isadie katika kusimamia suala hili. Alieleza kuwa hivi sasa miundombinu ya barabara ni mibovu hali inayosababisha magari mengi kukwama na kufanya magari yaliyoingia eneo hilo kushindwa kutoka.

"Anataka utaratibu uwekwe ili magari yaende kwa uchache. mimi nimeliafiki hilo hata Rais amekubali," alisema Bw. Pinda na kuongeza;

"Tunaomba mikoa yote nchini ituelewe. Kwa siku saba hatutaruhusu magari kwenda Samunge. Tumeandaa vituo vitatu ambapo magari yote yanayokwenda Samunge yatakusanyika. Vituo hivyo ni NMC Arusha mjini ambapo magari yanayotoka mikoa kama Dar es Salaam yatafikia. Kituo kingine ni Babati, Manyara na Kanda ya ziwa ni kituo cha Bunda, Mara."

"Vituo hivi vitakuwa na radio za mawasiliano na zikiruhusiwa zitapita Mto wa Mbu. Malori na mabasi mabovu hayataruhusiwa tunataka yaende mabasi mazuri yanayoweza kusafiri salama. Magari yote hayo yatapewa namba na kupakwa rangi maalum na yatakutana Mto wa Mbu."

"Polisi wajipange pawe na radio NMC, Babati, Bunda na Mto wa mbu. Ahudumie(Babu) alau wagonjwa 1,000-1,500 ili naye apate muda wa kupumzika tofauti na sasa ambapa anahudumia watu zaidi 2,000 kwa siku,"alisema Bw. Pinda

Alisema katika kuhakikisha huduma zinaimarishwa, serikali imeagiza Halmshauri ya Wilaya ya Ngorongoro kuhakikisha maeneo korofi barabara ya kwenda Samunge, yanakarabatiwa haraka sambamba na ujenzi wa vyoo vya kutosha na kupeleka bomba la maji eneo hilo.

Alisema mbali na hilo, serikali imeiagiza halmashauri hiyo kuboresha kituo cha afya kijijini hapo kwa kupeleka  dawa za kutosha ili kusaidia wagonjwa watakaohitaji dawa za hospitali sambamba na kuongeza maturubai nyumbani kwa Babu Mwasapile na kwenye zahanati hiyo ili kuwawezesha wagonjwa kupata eneo la kupumzikia.

"Tumegundua pia kuwa hapo kwake kuna tatizo la mazingira lakini kwa kuwa anatumia kuni kavu ambazo ukweli hazina athari ya mazingira, tumeagiza mamlaka ya halmashauri hapo wamsaidie. Sufuria na vikombe tutaongezea tukiona inafaa," alisema.

Bw. Pinda alisema serikali imechukua jukumu la kusaidia tatizo hilo kwa mtazamo wa kiutu na kwamba wanaokwenda ni wananchi wake kwa imani waliyonayo kuhusu tiba hiyo.

Matokeo ya utafiti wa dawa

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imesema kuwa dawa inayotolewa na Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri nchini (KKKT), Ambilikile Mwaisapile haina madhara yotote kwa binadamu.

Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Bi. Charys Ugullum alipokuwa akitoa matokeo ya utafiti walioufanya kuhusu dawa ya Babu wa Loliondo mjini Arusha kwa kushirikiana na taasisi nyingine zilizoko chini ya wizara hiyo.

Taasisi hizo mbali na TFDA, ni Taasisi ya Utafiti wa Dawa asili ya Chuo Kikuu Cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali (CGC) na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR).

"Awali jambo hilo lilizua hofu kwa serikali, wataala mbalimbali na Watanzania kwa ujumla," alisema. 

Bi. Ugullu alisema dawa inayotolewa Loliondo na Mchungaji Mwaisapile wameichunguza na kupata matokeo kutokana na kipimo anachotumia kutibu wagonjwa wameridhika nacho na haina madhara yoyote kwa sasa.

Alisema wao kama watafiti walichukua sampuli ya dawa ambayo haijatengenezwa na iliyotengenezwa ili kuifanyia uchuguzi katika maabala zao.

"Tuliichukua dawa hiyo na kuja nayo Dar es Salaam na kuifanyia uchunguzi na tumegundua kwamba ni salama.

"Sisi sote tuliofanya utafiti tumeridhishwa na dawa anayotoa Mchungaji Mstaafu Ambilikile Mwasapile," alisema Bi.Ugullum.

Hata hivyo alisema hatua ya uchunguzi itaendelea zaidi ili kubaini kama kweli dawa hiyo inatibu magonjwa matano kama alivyosema mchungaji huyo.

Aliongeza kuwa wanaendelea kufanya uchunguzi huo ili kujua kama dawa hiyo inafikia viwango na vigezo ambavyo vinakubalika  kitaifa na kimataifa kwa matumizi ya binadamu.

Alisisitiza kuwa katika uchunguzi huo ambao utachukua muda mrefu ili kupata matokeo, watafuatilia maendeleo ya wagonjwa 200 ambao wameshapata kikombe cha babu na kukubali  kupima afya  zao kujua maendeleo yao.

"Tutafanya utafiti kupitia kwa wale ambao wameshakunywa dawa ili tujue kama wamepona magonjwa yao waliyokuwa nayo," alisema.

Bi. Ugullum alisema sanjari na hilo wataendelea kufanya utafti na uchambuzi wa kisayansi katika maabala zao kwa kutumia sampuli waliyopewa na mchungaji huyo.

Aliongeza kuwa wao kama wadu wa afya wameandaa utaratibu madhubuti wa kufuatilia matumizi ya mti huo ambao unatambulika kama 'Carissaspinarum' katika sehemu nyingine za nchi yetu ili kujua kama ni mmea  wa tiba.

"Tuna taarifa kwamba kwa kipindi kirefu makabila mbalimbali yamekuwa yakitumia mti huo kama tiba. Tutafanya utafiti kwa Wagogo, Wamasai, Wabarbaig na Wasonjo wa kule Samunge ili kupata ukweli zaidi juu ya dawa hii," alisema.

Alitoa mwito kwa Watanzania kuwa wavumilivu kwa sababu tafiti za aina hii hazina njia ya mkato na kuahidi kutoa taarifa za kina kuhusu dawa hiyo mara tu watakapokamilisha utafiti wao.

Alimshukuru Mchungaji Mwasapile kwa ushirikiano aliouonesha kwa timu ya watafiti walioenda kumuona kutoka siku walipofika Loliondo.

Naye Msajili wa Baraza la Tiba Asili na Mbadala Daktari Paulo Mhane alisema wako katika hatua za mwisho kushughulikia usajili wa huduma ya mchungaji huyo ili  kupata cheti cha ukubalifu.

Msimamo kuhusu Gaddaff

Mbali na dawa ya Samunge, Bw. Pinda alisema Tanzania ina uhusiano mzuri na Libya hadi machafuko yalipoibuka nchini humo hivi karibuni. Alisema hadi sasa haijatoa msimamo wowote kuhusu kinachoendelea nchini humo na kwamba inasubiri msimamo utakazotangazwa na wakuu wa Umoja wa Afrika (AU)

"Njia rahisi ni kupitia AU. Tusubiri msimamo utakaotolewa na AU. Lakini kinachosikitisha ni kwamba binadamu wanaendelea kufa si jambo zuri sana, wakubwa watangulize utu kwanza," alishauri.

  Mikoa mipya

Alisema mchakato kwa ajili ya kuanzishwa mikoa mipya na  wilaya zake umekamilika na inatarajiwa kuanza kipindi cha mwaka ujao wa fedha. Alieleza kuwa kilichobaki ni tangazo kwa mujibu wa sheria na maoni ya Watanzania na kuweka tangazo hilo kwenye gazeti la serikali

 Matumizi ya mashangingi

Bw. Pinda alisema serikali inazidi kushughulikia suala la kupunguza magari ya kifahari serikali maarufu kama mshangingi na tayari ofisi yake imekwisha andaa viwango mbalimbali vya magari yanayopaswa kutumiwa na maofisa wa ngazi mbalimbali wa serikali.

 Malumbano ndani ya CCM

Kuhusu malumbano yanayoendelea ndani ya chama tawala CCM kati ya makada wake wakongwe na Umoja wa Vijana wa chama hicho, Bw. Pinda ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM, alisema anasikitishwa na hali hiyo.

Aliwataka wanachama wa CCM kutumia vikao na kutokuwa woga kutoa madukuduku yao ndani ya chama kwani hiyo ndio njia pekee ya kukijenga chama hicho.

"Nawasihi tutumie mfumo wa vikao vya chama na tusiwe woga huko ndiko sehemu ya kujenga. Mahali pazuri ni kutumia vikao vya chama...Mifumo mingine haitoi picha nzuri.

       Mgawo wa umeme
Alisema mvua zilizoanza kunyesha nyanda za juu Kusini zimeleta ahueni ya mgawo wa umeme kutokana na vyanzo vya Kidatu na Kihansi kupata maji ingawa Mtera bado kuna tatizo.

Hata hivyo alisema serikali inaendelea kuchukua juhudi mbalimbali kuhakikisha megawati 160 zinapatikana mwaka huu kupitia chanzo cha Ngaka na Mchuchuma na kubainisha kuwa  miaka miwili hadi mitatu ijayo, tatizo la umeme litapungua. 

  Malipo walimu wapya

Aliziagiza  halmashauri za wilaya kote nchini kuhakikisha zinatoa barua zinazoonesha stahili za walimu wapya waliopelekwa wilaya mbalimbali nchini na kuwalipa haki hizo

Ametoa agizo hilo kutoka na kile alichoeleza malalamiko anayopokea ofisini kwake kuhusu walimu hao 'kupigwa danadana' juu ya haki zao mbali ya kuripoti kwenye vituo vyao vya kazi.

"Tumepeleka posho zao, halmashauri zisiwababaishe, wawaambie stahili zao  kwa mujibu wa taratibu za utumishi serikalini. Wawaambie waziwazi au wawaandikie haki zao," aliagiza

Kuhusu maofisa kilimo na mifugo 2000 waliotarajiwa kuingia kwenye ajira Mei mwaka huu sasa wataunganishwa na wenzao wapatao 3000 na kuingizwa kwenye ajira katika mwaka ujao wa fedha unaonzia Julai mwaka huu.

9 comments:

  1. Kwanza nawapongeza wanasayansi kwa kazi mliyoianza, pili naomba kama kweli babu ndiye chimbuko la kuutangaza mti huo apewe hati miliki ili pale faida na dunia itakapoanza kuutambua mti huo na kuutumia, apate fedha zake isiwe kama wasanii wa Tanzania wanaofanyia kazi wengine. Pili babu acha ubinafsi wa maombi, omba Mungu ashukie walau mjukuu wako au mwanao atakayeweza kukaa hata arusha mjini ili wagonjwa wapate nafuu. Huyu Mungu asiyeona huruma wakati watu wengi wanakufa kwa ajali na wengi wanateseka baridi na usumbufu wa siku nyingi wakisubiri dawa, huyu atakuwa Mungu gani! Kama ndiye Mungu wa Israeli mwambie amuweke wakfu kama eliya alivyompa mkoba elisha. Ubarikiwe na poleni wagonjwa.

    ReplyDelete
  2. Mmnapoteza muda na fedha za walipa kodi kutoa ripot ambazo hazikidhi matakwa na hazina jipya,wananchi walichosubiri kwa hamu ni kujua kama kweli dawa hiyo inatibu au la,wacheni ubabaishaji toa taarifa sahii,kwani najua hata huyo wa Mbeya mtatoa taarifa kuwa DAWA YAKE HAINA MADHARA

    ReplyDelete
  3. Kumbe uwezekano wa kutengeneza miundombinu ulikuwepo, hakuna aliyekuwa anawajibika,
    ni hadi atokee babu ndio paboreshwe what a stpid leaders of these days

    ReplyDelete
  4. Muheshimiwa mnaanzisha Mikoa mipya hii tuliyonayo bado inawashinda maana kikatiba mnahitaji kuweka madhari nzuri kama mikoa kuwe na miundo mbinu, ubunifu wa ajira ili kulinda vijana kukaa na kufanya kazi mikoni mwao badala ya kukimbilia miji mikubwa lakini Tanzania yetu tunaona sehemu zinazoangaliwa kwanza wanakokaa wakubwa. Mimi bado najiuliza hivi mikoa yote ya tanzania zimo kwenye budget za serikali? Inakuwa vipi mikoa mingine toka uhuru inaonekana kama vijiji Mawaziri wakuu wangapi wamepita hawajali lakini wakikaa kwenye meza zao wameshiba, Unasikia nchi yetu kubwa bwana mikoa yazidi kuongezeka papo hapo watu watakapoleta malalamiko ya msingi kuhusu maendeleo ya mikoa yao hapo ndipo utakapoona misuli ya serikali. Kwa nini hii misuli yenu isutumike kuimarisha hiyo mikoa mliyoisahau Maana hawa viongozi huwa wakarimu sana wanapokuja omba kura na Ahadi kemkem Je hamuoni aibu? Mimi naona hii anzisha ya mikoa mipya na kuna watu tayari wameandaliwa ili nao wakatajirike huko Najua mnasema ili tulete maendeleo mikoni mwetu inabidi wazawa wawe mstari wa mbele Hakuna kitakacho fanyika bila nguvu ya serikali na matokeo yake ndiyo haya tuyaonayo Kuna baadhi ya miko inasikitisha hata kuitwa mikoa viongozi achaneni na porojo za siasa tunataka VITENDO.

    ReplyDelete
  5. Jamani hii serikali muflisi kabisa! Yaani mbele ya mataifa mengine tunaonekanaje? Hivi kama hii dawa inatibu ni kwanini serikali haichukui hatua ya kuiwasilisha shirika la afya duniani (WHO) ili ipate hati miliki na itengenezwe kwa wingi watu wapone na serikali ipate kodi? CCM acheni utapeli, hii si dawa bali mauzauza tu! Kwa kuwa mmekubali hii ngoja atokee shehe aseme naye kaoteshwa halafu tuone mtapeleka miundo mbinu, magari ya wagonjwa, n.k. huko? Hiyo tisa, kumi ni pale wagonjwa watakapoanza kufa na watu kuzinduka mtawaeleza nini wakati mmethibitisha inatibu? Ama kweli, nchi imeoza! lazima tuwaeleze ukweli nyie wakristo koko mliojaa serikalini kwamba mchezo wenu ni mauti yetu sote! Hubirini neno la mungu kanisani na si kuleta serikalini. Nyie si ndo mlikuwa wa kwanza kusema mahakama ya kadhi ni imani ya waislamu isitumie fedha za serikali? Sasa hii dawa wenyewe mnasema ni imani ya mtu iweje mdai kupewa huduma na serikali? Shwaaaaini nyie!

    ReplyDelete
  6. Naomba tusiingize swala la udini katika dawa ya Mchungaji Ambilikile Mwasapile. Dawa anayotoa haibagui kati ya Mkristo, Muislamu au pagani.

    Na wala Babu hajakuita uende kwake kunywa hiyo dawa. Uchaguzi ni wako.

    Wako watu wengi wenye kudai kuwa wanaombea watu wakapona: Kakobe, Lusekelo, Mwingira nk. Mbona hatujaona watu kufurika namna wanavyofanya kwa Babu? JIULIZE.Babu kawaumbua matapeli hawa.

    TIBA YA BABU HAINA UDINI; NI TIBA YA UKWELI NDO MAANA WATU WANAKWENDA HUKO.YAANI WOTE HAO NI WAJINGA?

    ReplyDelete
  7. Jamani kwa mujibu wa babu msingi wa uponyaji kwa dawa ya babu niimani.Watafiti mkitaka kuchunguza tiba hii fanyeni utafiti kama imani kwa Mungu inaweza kumponyesha mtu!. Nadhani kwenye utafiti wenu mtagundua kuwa kwa dawa hiyo hiyo wengine watapona kabisa hao wenye imani na wengine hawatapona wasiokuwa na imani hasa wale wanaosubiri wanasayansi wathibitishe!. Maana hao watawaamini wanasayansi na siyo Mungu aliye nyuma ya uponyaji unaohubiriwa na babu.

    ReplyDelete
  8. MI OBBELINE THOMSON nipo huku TABORA ki masomo,napenda kuwapongeza waandishi wote wanao ipa kipaumbele suala la ugunduzi wa dawa hizi asilia. Lakini Jamani mbona mi naona kwa hali hi kweli kama si kupona wengi tutaangamia wengi.HEBU na hawa viongozi wetu wawe wanawaza mara kumikumi. MNATUPELEKA PA BAYA.LEO hii kila mtu anataka kuwa mganga wa magonjwa sugu. WATANZANIA WENZANGU NAWAOMBA SANA MUWE NA AKILI NA HEKIMA YA MUNGU.JAPO HAWA WAKUBWA WETU NAO WANATUSHAWISHI.

    ReplyDelete
  9. Mkemiamkuu wa serikali hana budi kujihuzulu na viongozi wengine waandamizi.Sababu anadhibitisha dawa ya babu kuwa haina madhara wakati watanzania wengi wamekwisha kunywa,ingekuwa na madhara tungepoteza Watanzania wengi wasio na hatia.Tafakari..........BY BONAVENTURE

    ReplyDelete