30 July 2013

WATUMISHI WANAOTOA LUGHA CHAFU KUADHIBIWA



Na Moses Mabula, Tabora
SERIKALI wilayani Tabora imeahidi kuwachukulia hatua kali za kinidhamu watendaji wa kata na mitaa watakaobainika kuwatolea lugha chafu wananchi wanaoenda kutafuta huduma muhimu za kijamii katika ofisi za Serikali.

Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa na Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Selemani Kumchaya, wakati akizindua mradi wa kutoa huduma ya msaada wa kisheria kwa makundi yenye uhitaji unaotekelezwa na Shirika la Tabora Paralegal Centre.
Akizungumza katika hafla hiyo mkuu huyo wa wilaya alisema kwamba kuanzia sasa mtendaji yoyote atakayebainika kumnyanyasa mwananchi kwa hila atamchukulia hatua kali za kinidhamu ikiwa ni pamoja na kumfukuza kazi.
Alisema kwamba ofisi yake imekuwa ikipokea malalamiko mengi kila mara kutoka kwa wananchi dhidi ya watendaji na kuonya kuwa tabia hiyo iachwe mara moja.
"Hapa Tabora bado kunatatizo kubwa sana la ardhi, hivyo nitoe wito kwa maofisa ardhi, mshirikiane na madiwani kutatua haraka tatizo hilo," alisema Kumchaya.
Awali Mwenyekiti wa bodi ya Paralagal Centre, Betha Kayila alisema kuwa shirika lake litatekeleza mradi wa miaka miwili 2013 na 2015 wa kutoa huduma ya msaada wa kisheria kwa makundi yenye uhitaji kama vile wanawake, wazee, watoto na wanaume watakaohitaji msaada huo.
Alisema lengo la mradi huo ni kuwezesha jamii kupata huduma ya msaada wa kisheria ambazo zimekuwa zikipotea au kushindwa kupatikana kutokana na jamii kukosa huduma ya msaada wa kisheria kwa sababu mbalimbali ikiwemo ukosefu wa fedha wa kumlipa wakili.
Aidha alisema kuwa lengo lingine la mradi huo ni kupanua wigo wa huduma za msaada wa sheria katika kata 16 za Manispaa ya Tabora ambapo wakazi wake katika eneo la mradi, watawezeshwa na kujengewa uwezo wa kufuatilia haki zao kwa kuzingatia utawala wa sheria unaopewa kipaumbele na Serikali iliyopo madarakani.

No comments:

Post a Comment