Na Lilian Justice, Morogoro
WANAFUNZI 600 wa
Sekondari ya Junior S e m i n a r y i l i y o p o Manispaa ya Morogoro
wameandamana kutoka shuleni hadi ofisi ya Askofu Mkuu wa Kanisa la Kilutheri
Dayosisi ya Morogoro, Jacob Mameo kwa madai ya kutaka kuondolewa kwa mkuu wa
shule hiyo Laiser Saningo kutokana na uongozi wake mbovu uliosababisha matokeo
mabaya.
Wakizungumza na wanahabari kwa kutokutaja majina yao walisema kuwa
ni muda mrefu wamekerwa na uongozi wa shule kiasi ambacho kumechangia shule
hiyo kufanya vibaya katika matokeo ya kidato cha nne na sita katika miaka
mitatu iliyopita.
Aidha wanafunzi hao walisema kuwa shule hiyo ina matatizo ya
upungufu wa vitabu vya biologia na pindi wanapouliza kwa uongozi wa shule
wanaambiwa shule inatafuta pesa,ukosefu wa kiu ya taaluma imeshuka kutokana na
walimu kutokuwa na mwamko wa kutoa mitihani ya majaribio ya mara kwa mara
inayowafanya kufanya vizuri katika mitihani ya mwisho.
"Walimu wetu hawamalizi mitaala kwa muda unaotakiwa hususan
vidato vya nne na sita, kutopewa mitihani ili kujifunza hivyo kupelekea matokeo
kuzidi kushuka kama yalivyo matokeo ya kidato cha sita 2013 na hii inatokana na
walimu hawapewi motisha wa kufundisha," walisema.
Pia walibainisha kuwa wanafunzi wa kidato cha nne walikaa kikao na
mkuu wa shule na kumuuliza swali kuhusu mitihani ya ndani na nje lakini
walishangazwa na jibu lililotolewa ni kwamba shule haina pesa jambo ambalo
linawakatisha tamaa kutokana na ada kubwa inayolipwa na wazazi wao.
Waliongeza kuwa jambo lingine ni kubadilishwa ghafla kwa sheria za
shule bila ya maelezo yoyote kutoka kwa uongozi na hivyo kuwa kandamizi na
baadhi ya sheria hizo zinawapa mashaka uongozi wa shule unatumia kuficha maovu
yao kwa wanafunzi kutokana na wawakilishi katika vikao vya shule ni walimu na
sio Serikali ya wanafunzi
Pia walidai kuwa kusikitishwa na walimu kuendeshwa kidikteta na
uongozi wa shule na kusababisha baadhi yao kuondoka na kushindwa kusimamia
wanafunzi ipasavyo na hatimaye kutafutwa walimu wengine ambao hawana sifa za kufundisha
wala za ualimu na kufanya taaluma kuporomoka kila mwaka.
Madai mengine ya wanafunzi hao ni kukosekana kwa dawa katika
zahanati ya shule, uchache wa wauguzi, chakula maalumu cha wagonjwa, vitanda
vichache vya wagonjwa, kutokuwepo kwa madaktari siku za Jumapili na Jumamosi,
hali hii inachangia kwa kiasi kikubwa afya za wanafunzi kuwa matatani pindi
kunapotokea magonjwa ya mlipuko.
Kwa upande wake Askofu wa Kanisa la Kilutheri Dayosisi ya
Morogoro, Jacob Mameo akizungumza na wanafunzi hao katika Kanisa la Mji Mpya
mjini humo alisema kuwa maandamano waliyofanya wanafunzi hao wametumia njia
halali ya kudai haki zao pasipo kufanya vurugu wala kuharibu mali za shule na
umma kwa ujumla.
Askofu Mameo alisema kuwa bodi ya shule itakaa na kutatua kero
hizo za wanafunzi mapema ili kuwafanya kuweza kuendelea na masomo yao kwa
kufuata taratibu na sheria za shule zilizowekwa zikiongozwa na Kanisa hilo.
Mameo ambaye pia ni Mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo alisema kuwa
madai ya wanafunzi hao yana ukweli ndani yake na kuahidi yeye na bodi kuyapatia
ufumbuzi haraka, suala la mwalimu mkuu watamuondoa kwa kufuata taratibu na
sheria kutokana na kuonekana hawezi kuongoza shule hiyo.
Hata hivyo wanafunzi hao walianza
maandamano jana saa 5.30 asubuhi wakitoka eneo la shule hiyo iliyoko nje kidogo
ya manispaa pasipo walinzi na walimu kujua wanakoelekea, ikiwa ni mara ya pili
wanafunzi hao kudai haki zao, mara ya kwanza walifanya mgomo mwaka jana na
mwaka huu wameamua kufanya maandamano ya amani.
No comments:
Post a Comment