29 July 2013

WASOMI, WANASIASA WALIA NA SERIKALI



Na Mwandishi Wetu
WASOMI na wanasiasa nchini wameishukia Serikali kuwa ndiyo inayochangia hali ya kuhatarisha amani ya nchi na kwamba hali hiyo ikiendelea hivyo miaka 50 ijayo Tanzania haitakuwa kisiwa cha amani tena.Walitoa kauli hiyo kwenye kongamano lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuhusu mustakabali wa amani na usalama wa taifa letu miaka 50 ijayo
. Walidai kuwa jinsi Serikali inavyotumia vyombo vyake vya dola kukandamiza wananchi wana imani miaka 50 ijayo amani haitakuwepo nchini.Mmoja wa wanasheria, Lilian Wassira, alisema kinachoponza Watanzania ni woga kiasi cha kuwafanya washindwe kudai haki zao. "Watanzania wasingekuwa woga wangeibana Serikali hadi kuiondoa madarakani," alisema. Kuhusu vikundi vya ukakamavu, alisema haoni shida kila chama kuwa na vikundi hivyo.
"Mbona vyama vingine vinavyo, wao wanahofia nini?" Alihoji. Kwa upande wake mbunge wa CHADEMA, Tundu Lissu, alisema pamoja na Tanzania kuitwa kisiwa cha amani, lakini yeye anaiona kama kisiwa cha ukandamizaji.Alitoa mfano kuwa mwaka 1967 wakati wa kuanzisha vijiji vya ujamaa kuna watu waliwekwa ndani. Alisema kuwa hata mwaka 1980 kuna watu waliwekwa ndani walipohoji uhalali wa Muungano. Lissu alisema kwenye miaka ya 1980 kuna watu waliondolewa kwenye vijiji vyao ili kupisha uchimbaji wa madini.
Alisema anawashangaa wasomi kutozungumzia masuala hayo badala yake wamejikita kwenye suala la ajira. Kwa upande wa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Willbrod Slaa, alisema anamshangaa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi (Dkt. Emmanuel Nchimbi) kutojiuzulu wakati jeshi la polisi linaongoza kwa kuvunja haki za wananchi.
Alitoa mfano mauaji ya mwandishi wa habari, Daud Mwangosi, kuwa hadi sasa hakuna ripoti iliyotolewa huku twiga wakiibwa na kusindikizwa na askari. Alisema Mtwara kuna uvunjifu wa amani na wanaofanya hivyo ni vyombo vya dola."Chanzo cha kupotea kwa amani itakuwa ni jeshi la polisi," alisema. Naye Profesa Mpangala, alisema chama tawala kisipojiondoa kwenye dola miaka 50 ijayo Tanzania haitakuwa tena kisiwa cha amani.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro, anasema tunapoelekea Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) linaelekea kupoteza sifa. Alitoa mfano kuwa viongozi wa chama hicho walipigwa na JWTZ, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa

No comments:

Post a Comment