Na Mwandishi Wetu, Mwanza
WAKAZI wa Mwanza
na vitongoji vyake juzi walishuhudia vitu tofauti wakati wa uzinduzi wa Tamasha
la Filamu la Wazi la Grand Malt Tanzania, ulioongozwa na Mkuu wa Wilaya ya
Busega, Paul Mzindakaya, lililofanyika kwenye Uwanja wa Nyamagana, jijini hapa.
Tamasha hilo maarufu kama 'Grand Malt
Tanzania Open Film Festival' lilinogeshwa zaidi na burudani kali kutoka kwa
bendi ya Extra Bongo, waliokuwa wakiongozwa na Ally Choki.
Shamrashamra za uzinduzi huo
zilionekana toka mapema alfajiri, wakati wasanii wa Bongo Movie walipojikuta
wakibanwa kila mahali walipokuwa wakipita kutambulisha ujio wao.
Wakati wa uzinduzi huo, wasanii
waliokuwepo uwanjani hapo wakiongozwa na Hashima Kambi, walijikuta wakizongwa
kwa muda wote, huku mashabiki wakitaka kuwashika au kupiga nao picha.
Aunty Ezekil, Irene Uwoya, Jacqueline
Wolper, Vicent Kigosi 'Ray' na Jacob Steven 'JB' walijikuta wakishangiliwa muda
wote kama ilivyokuwa kwa Hashim Kambi, Isa Musa 'Cloud' na Steve Nyerere.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo,
Mkuu wa Wilaya ya Busega, Paul Mzindakaya, alisema amefurahishwa mno na tamasha
hilo na hasa watu waliokuwa wamejitokeza kwa wingi kushuhudia wasanii wao.
"Serikali itaendelea kuthamini kwa
kiasi kikubwa wasanii wetu na huu ni wakati wa wasanii wa Mwanza kujifunza
kutoka kwa mastaa wetu hawa," alisema.
Meneja wa
kinywaji cha Grand Malt, Consolata Adam alisema, wameamua kulidhamini tamasha
hilo kwani wanajua watu wengi kwa sasa wanapenda kutazama filamu za Tanzania.
No comments:
Post a Comment