Na Elizabeth Mayemba
KIUNGO mshambuliaji wa timu
ya Taifa Tanzania, Taifa Stars Mrisho Khalfani Ngassa
ni miongoni mwa wachezaji walioanza mazoezi jana asubuhi kwenye Uwanja wa Shule
ya Sekondari Loyola Mabibo, Dar es Salaam kwa ajili ya kujiandaa na msimu mpya
wa Ligi Kuu ya Vodacom 2013/2014 na mashindano ya kimataifa.
Ngassa ameanza
mazoezi ambapo hivi karibuni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kupitia kwa
Msemaji wake Boniface Wambura alisema wanatambua kama mchezaji huyo ni wa Simba
kwa kuwa Yanga haikupeleka mkataba wa mchezaji huyo ndani wa shirikisho hilo.
Pia Kocha Mkuu
wa timu hiyo Ernest Brands naye jana alitua nchini na kuungana na timu yake
mazoezini. Kocha huyo alikuwa kwao Uholanzi kwa ajili ya mapumziko.
Yanga ilikuwa na
mapumziko ya zaidi ya wiki mbili tangu kuahirisha kushiriki mashindano ya Kombe
la Kagame kufuatia serikali kuzizuia timu za Tanzania kwenda kushiriki
mashindano hayo kufuatia kuwepo kwa hofu juu ya hali ya usalama katika mji wa
Darfur nchini Sudan.
Mbali ya Ngassa
pia mshambuliaji Shaaban Kondo aliyejiunga na Yanga kama mchezaji huru akitokea
nchini Msumbiji alifanya mazoezi pamoja na wachezaji wengine wote wa klabu
hiyo.
Leo Yanga
wataendelea na mazoezi asubuhi kwenye uwanja wa Loyola ambapo golikipa mpya
aliyesajiliwa kutokea klabu ya Azam Deogratius Munishi 'Dida' ataungana na
wachezaji wengine katika mazoezi hayo ya kujiandaa na msimu mpya wa 2013/2014.
Wachezaji wengine waliofanya mazoezi
jana ni Ally Mustapha 'Barthez', Juma Abdul, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, David
Luhende, Nadir Haroub 'Cannavaro', Salum Telela, Didier Kavumbagu, Jerson
Tegete, Abdallah Mnguli, Nizar Khalfani na Frank Domayo.
Ijumaa Yanga watasafiri kuelekea Kanda ya Ziwa kwa ajili ya
kulitembeza kombe la Ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom pamoja na kucheza michezo
kadhaa ya kirafiki.
No comments:
Post a Comment