03 July 2013

STARS WAANZA MAANDALIZI CHAN


 Na Fatuma Rashid

TIMU ya Tanzania, Taifa Stars inatarajia kuanza kambi leo kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wao dhidi ya Uganda michuano ya wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN).
Akizungumza Dar es Salaam jana Kocha wa Stars, Kim Poulsen alisema kuwa mechi hiyo itachezwa Julai 13, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na timu yake itaweka kambi hoteli ya Tansoma jijini.
Poulsen aliongeza kuwa katika mechi hiyo dhidi ya Uganda wanaahidi kufanya vizuri, kwani hii ni mechi muhimu sana licha ya kuwa wachezaji wawili ambao ni Mbwana Samata pamoja na Thomas Ulimwengu hawatokuwepo ila ataimarisha kikosi chake vizuri.
Alisema licha ya mchezo huo kuwa mgumu kwao kutokana na timu ya Uganda kuwa na wachezaji wazuri, lakini watajitahidi kwani mazoezi ndio kila kitu.
"Najua mchezo huu utakuwa ni mgumu kutokana na wachezaji wa timu ya Uganda kuwa wazuri, lakini safu yangu ya ulinzi nitaipanga vizuri,"alisema.
Timu hizo zitarudiana baada ya wiki mbili, ambapo Stars watasafiri kuelekea Mwanza kwa ajili ya mazoezi kabla ya kwenda Uganda kucheza mchezo huo wa marudiano.

No comments:

Post a Comment