30 July 2013

WANNE WAFA MATUKIO TOFAUTI MOROGORO



 Na Lilian Justice, Morogoro
JUMLA ya watu wanne wamefariki dunia mkoani Morogoro katika matukio tofauti likiwemo la mmoja kuanguka juu ya mti wakati akikata kuni na mwingine kufa baada ya kushuka kwenye gari ili ajisaidie. Akizungumzia kutokea kwa matukio hayo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile alisema kuwa tukio limemhusisha Nailon Chipela (64), mkazi wa Kiburugutu Mngeta wilayani Kilombero kufariki baada ya kuanguka kutoka kwenye mti wakati akikata kuni.

Aidha alisema kuwa tukio hilo lilitokea Julai 28, mwaka huu, saa 5 asubuhi katika kijiji hicho ambapo marehemu huyo alidondoka na kuvunjika shingo pamoja na ubavu wa kushoto na kufariki papo hapo. Akizungumzia tukio la pili alisema abiria aliyefahamika kwa jina la Fredy Kiuma (30), mkazi wa Mbagala Dar es Salaam alifariki dunia baada ya kushuka kwenye basi ili ajisaidie, ambapo alikuwa akisafiri na basi lenye namba T 758 BZD mali ya Kampuni ya Njombe Expres.
Pia alisema basi hilo lilikuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea Iringa na kwamba ilitokea Julai 26, saa 3:30 asubuhi katika eneo la ATN Msamvu mjini Morogoro, huku chanzo cha kifo hicho kikiwa bado hakijafahamika na polisi wanaendelea na uchunguzi.
Kamanda Shilogile alisema tukio la tatu lilitokea Julai 26, saa 3 asubuhi huko Misufini tarafa ya Mang'ula wilayani Kilombero likimhusisha Juma Nguwa (26), mkazi wa Kiberege Wilayani humo kukutwa ameuawa na watu wasiojulikana.
Alisema mtu huyo alikuwa na majeraha sehemu za shingoni, paja la mguu wa kushoto na jicho la kulia yanayoonesha kuwa alipigwa na kitu chenye ncha kali, na kwamba katika uchunguzi wa awali inadaiwa kuwa alienda kuiba kwenye gereji ya Makota.
Hata hivyo Kamanda huyo alisema katika tukio lingine mwendesha pikipiki, Gido Simba (40), mkazi wa Kibaoni alifariki dunia baada ya kugongwa na gari katika eneo la Kibaoni Ifakara wilayani Kilombero, ambapo aligongwa na gari namba T949 BPL Mistubish Fuso ikiendeshwa na Rashid Sultani, mkazi wa Mbagala Dar es Salaam, chanzo mwendokasi wa dereva wa gari hilo.  

No comments:

Post a Comment