Na Timothy Itembe, Tarime
MKUU wa Mkoa wa Mara, John Tuppa amewataka wananchi wa mkoa huo
kudumisha amani na kutojengeana chuki ambazo zitasababisha uhasama na
kusababisha mapigano ya koo na kutaka amani iliyopo sasa wilayani Tarime
iendelee kudumishwa. Hayo aliyasema jana mbele ya wananchi wa Kijiji cha Mugabiri
wakati wa mazishi ya Mwanajeshi wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), Peter Muhiri
Werema aliyefariki huko Darfur.
Tuppa alisema kuwa iwapo wananchi wa Mara watavunja amani na kuwa
na ubaguzi wa kabila na dini ni kiashirio kuwa siku moja Watanzania wakalindwa
na watu wa Mataifa na huenda vikatokea vifo kama kilivyotokea cha mwanajeshi
huyo Mtanzania na wenzake aliyefia huko Darfur nchini Sudan wakati akitekeleza
majukumu yake ya kazi.
Naye Luteni Dickson Mnubi kutoka kikosi cha 44 KJ Mbalizi Mbeya
alikokuwa akifanya kazi marehemu Werema akisoma wasifu wa marehemu alisema kuwa
marehemu alizaliwa mwaka 1984 na alijiunga na Jeshi Machi 2007 na katika
utumishi wake alihudhuria kozi ya mafunzo ya awali-RTS Makutopora -2007,
mafunzo ya askari wa miguu daraja la tatu-44 KJ- 2007, mafunzo ya askari wa
miguu daraja la pili- 42 KJ 2008 na kozi ya Polisi Jeshi Daraja la tatu- 832KJ
-2010.
Luteni Mnubi alisema kuwa madaraja aliyowahi kuhusika wakati wa
utumishi wake alishika madaraka ya polisi jeshi kitengo cha MP Section ambapo
pia alitunukiwa medali ya miaka 40 ya JWTZ ya kuthamini mchango wake katika
jeshi hadi hapo alipofariki Julai 14 huko Darfur
akitekeleza majukumu yake ya kazi.
Kwa upande wake mke wa marehemu Mary Peter (27) alisema kuwa kifo
cha mumewe huenda akaishi maisha magumu yeye na watoto wake 3 wa kike
aliowaacha kwakuwa mama huyo hakuwa na kazi yoyote ya kufanya alikuwa ni mama
wa nyumbani.
"Mume wangu ameniacha na watoto wadogo mwisho wa kuonana naye
akiwa hai ilikuwa Februari 7, 2013 kafa bila hata kuniambia chochote mimi mkewe
sina kazi sijui nitaishi vipi kwani hata huko Mbeya tulikuwa tunaishi kwenye
nyumba za jeshi," anasema mama huyo kwa uchungu.
Mary aliiomba Serikali kumjali
yeye na familia yake kwakile alichoeleza kuwa mumewe kafa akiwa kazini tena
akitekeleza majukumu ya kazi nje ya nchi yake hivyo yeye na familia yake ni
vyema wakalipwa haki stahili za mume wake ili ziwakwamue kimaisha na wala
wasiwepo watu wa kuingilia na kunyang'anya mirathi ya mumewe.
.
No comments:
Post a Comment