26 July 2013

SHEREHE SIKU YA MASHUJAA ZADODA



Na Elizabeth Joseph, Dodoma
MA A D H IMI S H O y a kumbukumbu ya Siku ya Mashujaa Mkoa wa Dodoma yameingia doa baada ya kukosa msisimko wa kutosha kutokana na maandalizi duni. Hali hiyo ilijitokeza siku ya jana katika maadhimisho hayo ambapo mwitikio wa wananchi haukuwa wa kutosha hali iliyosababisha baadhi ya watu kuhoji na wengine kulalamika kutokuwa na taarifa mapema.

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoa wa Dodoma, Job Lusinde akielezea siku hiyo alisema kuwa kwa kipindi cha miaka ya hivi karibuni kumekuwa na msisimko mdogo tofauti na zamani na kuongeza kuwa juhudi inahitajika kufanywa ili kuwaenzi vyema mashujaa hao.
Aidha Lusinde alikemea na kulaani kitendo cha baadhi ya wanasiasa wanaochochea umwagaji damu nchini na kusema wanapaswa kuacha mara moja kwani kwa kufanya hivyo amani na umoja wa nchi yetu vita itatoweka.
Naye Meja Jenerali Mstaafu Johnick Risasi ambaye pia alishiriki katika vita hiyo ya Kagera alisema kuwa ameangushwa na msisimko mdogo wa maandalizi hayo kwakuwa Manispaa ya Dodoma pamoja na wananchi wake wanapaswa kuenzi siku hiyo.
Risasi aliongeza kuwa Serikali pia inatakiwa kuandaa utaratibu wa kutenga eneo maalum ikiwemo makaburi ya mashujaa hao waliotangulia kwa kuyahifadhi vizuri pamoja na kuwajali watu waliopata ulemavu katika vita hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rehema Nchimbi aliwataka wananchi kuyaenzi maadhimisho hayo kama darasa la kujifunzia na kujiuliza wanawaheshimu vipi mashujaa hao waliotangulia pamoja na kuwataka kutii sheria bila shuruti kwa kuwaenzi bila kumwaga damu kwa kudumisha uhuru, umoja, upendo na amani ambavyo vililetwa na mashujaa hao.

No comments:

Post a Comment