02 July 2013

WANAFUNZI WAOMBEWA UJUZI KWA WAAJIRI


 Na Rehema Maigala

WAAJIRI wenye viwanda nchini wametakiwa kujitokeza na kushiriki katika kazi ya kutoa elimu na mafunzo ya ufundi stadi kwa wanafunzi ili kuwaongezea ujuzi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam katika maonyesho ya Biashara ya 37 ya Kimataifa, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Zebadiah Moshi alisema waajiri wasaidie kutoa mafunzo kwa wanafunzi katika kujifunza stadi zao kwa vitendo.


"Wanafunzi wanapata shida katika kipindi cha kujifunza kwa vitendo, kwani waajiri wengi wanakuwa hawatoi mwanya kwa wanafunzi kuingia katika viwanda kwa ajili ya kupata elimu ya vitendo," alisema Moshi.
Alisema kuwa, wafanyakazi wa viwandani wawe bega kwa bega katika utoaji wa elimu ili kufanikisha elimu kwa vijana.
Aidha, alisema wafanyakazi wanatakiwa kuingia madarasani kwa ajili ya kutoa elimu kwa wanafunzi na kuwasiliana na walimu juu ya uandaaji wa mitaala na ufundishaji.

"Teknolojia ya sasa ni ile inayobadilika, hivyo ni vizuri wafanyakazi wa viwandani kushirikiana na vyuo vya ufundi katika utoaji wa elimu hasa kwa kile kipya ambacho kinachojitokeza katika ulimwengu huu," alisema Mosha.

No comments:

Post a Comment