02 July 2013

TAPELI AWACHIMBISHA KABURI WATU, AIBA


 Na John Gagarini, Kibaha

MTU mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Abdul Ramadhan (35) amewatapeli baadhi ya wakazi wa Kwa Mathias wilayani Kibaha Mkoa wa Pwani kwa kuwachimbisha kaburi kisha kutoweka.
Aidha, mtu huyo aliwaachia kaburi tupu bila kuzikwa marehemu kama alivyowaomba azike ndugu yake.
Tukio hilo lilitokea juzi kwenye mtaa huo baada ya mtu huyo kufika hapo na kuomba kusaidiwa kumzika mfanyakazi wake ambaye alidai kuwa hana uwezo wa kumsafirisha kwani kwao ni mbali.

Mbali ya kuwachimbisha kaburi wakazi hao pia alifanikiwa kuwaibia simu mbili pamoja na kamera moja na kuwaachia deni kwenye vyakula ambavyo vilitumiwa na wachimba kaburi huku kingine kikiwa kimeandaliwa bila ya kuliwa.
Akielezea mkasa huo Ustaadhi wa Masjid Kadiriya uliopo Kwa Mathias, Said Omary alisema kuwa, mtu huyo alifika msikitini hapo na kukutana na kiongozi kisha kuomba kuwa asaidiwe kuzikiwa mfanyakazi wake msikiti ukamkubalia na taratibu zikaanza kufanyika.


Omary alisema kuwa, baada ya kuelekezwa na mkuu wake alitakiwa ashughulikie suala hilo na kwenda na mtu huyo kwenye makaburi ya mambo akiwa na watu wengine watatu kwa ajili ya kuchimba kaburi kwa ajili ya kumsitiri marehemu.
"Tulikwenda makaburini na wachimbaji wakaanza kazi ya kuchimba kaburi akawaletea chai na maandazi 20 wakanywa wakaendelea na kazi yao, mimi akaniambia twende Hospitali ya Tumbi aliko marehemu kwa ajili ya kumwandaa," alisema Omary.

Alisema, wakiwa njiani alimwambia kuwa anaomba simu yake ili awasiliane na ndugu zake kwani ya kwake imeisha chaji pia amtafutie mpigapicha kwa ajili ya tukio hilo kwa ajili ya kuwaonyesha ndugu juu ya mazishi hayo.
" Tu l i kwe n d a kwa mp i g a p i c h a wakakubaliana apige picha akasema kabla ya kwenda Tumbi wakachukue nyama na vitu vingine kwa ajili ya msiba huo na walipofika Maili Moja wakachukua nyama kilo 25," alisema Omary.
Aliongeza kuwa, wakati wameshapima nyama aliwaambia ngoja akanunue viungo vingine lakini hakurudi tena na kutoweka kusikojulikana huku kaburi likiwa limeshachimbwa na liko wazi hadi sasa.

Kwa upande wake mpigapicha Juma Said ambaye yeye aliibiwa kamera na simu alisema kuwa, walikubaliana apige picha 36 hadi 40 ambazo gharama yake ni sawa na sh. 36,000 au 40,000.
Alisema, wakati wako kwenye harakati ya kununua nyanya alimwachia begi likiwa na kamera na simu lakini aliporudi hakumkuta akiwa yeye na Ustaadhi na dereva wa teksi ambayo aliikodisha kwa shughuli za mazishi hayo.
"Alituacha mimi na ustaadhi tukiwa na nyama huku tukimsubiria hali ambayo ilitufanya tuingie matatani kwani wauzaji nyama ilibidi watubane ndipo tulipowaelewesha juu ya hali halisi ndiyo ikawa salama kwetu na kuondoka," alisema.
Watu waliokumbwa na hali hiyo walisema kuwa mbali ya kudanganya mambo yote hayo pia tapeli huyo aiagiza chakula sahani 20 kwenye hoteli lakini hakuonekana tena.

"Katika kufuatilia walibaini jina la mtu huyo, kwani siku moja kabla ya tukio hilo alilala kwenye nyumba ya kulala wageni ya Iwawa iliyopo Mtaa wa Kwa Mbonde jirani na hapo wakazi hao walitoa taarifa kwenye Kituo cha polisi Kwa Mathias juu ya tukio hilo," alidai mkazi mmoja.

No comments:

Post a Comment