29 July 2013

TUICO YAKOSOA MFUMO WA ELIMU NCHINI



 Na Grace Ndossa
CHAMA cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara Taasisi za fedha, Huduma na Ushauri (TUICO) kimekosoa mfumo wa elimu nchini kwa kile kilichoelezwa kuwa haukidhi matakwa ya soko la ajira duniani
.Pia kimesema kuwa mfumo wa elimu uliopo hauzalishi wataalamu wa kutosha wa fani mbalimbali wanaoweza kufanya kazi kwa weledi katika sekta mbalimbali ndiyo maana kwenye sekta binafsi nchini, kazi nyingi za juu zinafanywa na wageni huku Watanzania wakiendelea kubaki katika ajira zisizo na uhakika.
Hayo yalibainishwa mwishoni mwa wiki na Katibu mKuu wa TUICO, Boniface Mkakatisi, alipokuwa akizindua baraza la Katiba la chama hicho. Alisema asilimia kubwa ya kazi zenye kuhitaji ujuzi na sifa za juu zinaendelea kufanywa na wageni huku Watanzania walio wengi wakibaki hawana kazi.
"Pamoja na mapitio ya rasimu ya katiba, nchi yetu haina budi kufanya mabadiliko makubwa katika sekta ya ajira , lazima Serikali ikubali mfumo wa elimu uliopo haukidhi matakwa ya soko la ajira duniani," alisema Mkakatisi.
Alisema rasimu ya katiba mpya inatakiwa kuhakikisha kuwa ajira za kutosha zinatengenezwa, mazingira ya kazi yanaboreshwa na wafanyakazi wanalipwa ujira na mishahara yenye staha kwa ajili ya kuwawezesha kumudu gharama za maisha pamoja na kuwapa morali wa kufanya kazi.
Hata hivyo alisema kuwa pamoja na ugumu wa mazingira ya kazi, mishahara duni na hali ngumu ya maisha bado kipato cha mfanyakazi kinaendelea kupungua kutokana na kiwango kikubwa cha kodi ambayo ni chanzo kimojawapo cha Serikali katika mapato.
Mkakatisi alisema vyama vya wafanyakazi vimewahi kutoa maoni mwaka jana na walipendekeza kiwango cha malipo ya kodi kipungue kutoka asilimia 14 hadi 9.

No comments:

Post a Comment