02 July 2013

TRENI YA MWAKYEMBE YAPATA AJALI


UONGOZI wa Kampuni ya Reli nchini (TRL) umesitisha kutoa huduma ya usafiri wa treni kutokana na vichwa viwili kupata ajali iliyotokea jana asubuhi eneo la Kamata, Kariakoo, anaripoti Stella Aron.

Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na TRL kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Mhandisi Kipallo Kisamfu, alisema kichwa kimoja kiligongwa na roli la mizigo aina ya Fuso katika makutano ya barabara hiyo.

Katika ajali hiyo, dereva wa Fuso alifariki dunia papo hapo na utingo wake alinusurika.

Aliongeza kuwa, kichwa kingine kiligongwa na daladala aina ya Isuzu ambapo baadhi ya abiria wa basi hilo walijeruhiwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wakiwemo askari wawili wa Kikosi cha Reli mmoja akiwa mahututi.

Aliongeza kuwa, kutokana na ajali hizo huduma za treni zilisimama kwa muda na kuwepo kwa mabadiliko ya ratiba yaliyochangiwa na ujio wa Rais Barack Obama wa Marekani.

Alisema uongozi wa TRL umetoa taarifa kwa wakazi wa jiji hilo juu ya kusitishwa huduma ya treni siku ya leo hadi kesho ambapo zitarejea kama kawaida.

1 comment:

  1. JAMANI TUUJALI UHAI WETU. KULIKO KITU KINGINE CHOCHOTE.

    ReplyDelete