29 July 2013

TANZANIA KUPAA KIUCHUMI 2025



Na Fatuma Mshamu
SERIKALI kupitia Ofisi ya Rais Tume ya Mipango imesema hadi kufikia mwaka 2025 Tanzania itafikia hadhi ya nchi zenye kipato cha kati na kuondokana na umaskini uliokithiri.Hayo yameelezwa jana Jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Joyce Mkinga alipokuwa akifafanua juu ya mpango wa maendeleo wa mwaka 2025. Alisema, malengo makuu ya mpango huo ni kuwaletea wananchi maisha bora kudumisha utawala wa sheria na kujenga uchumi imara wenye uwezo wa kukabiliana na ushindani
.Alisema matokeo ya mapitio ya Dira ya Taifa ya maendeleo yameonyesha mafanikio katika kujenga uchumi imara na ushindani ambapo uchumi ulikuwa kwa asilimia 6.5 ukilinganisha na asilimia 8 kwa nchi za kipato cha kati."Matokeo haya yanaonyesha kuwa dira hii haikutekelezwa ipasavyo na ili kuimarisha utekelezaji wake, Serikali ilifikia uamuzi wa kurejea katika uundaji wa mipango ya muda mrefu (miaka 5) kama chachu ya utekelezaji na uimarishaji mipango hiyo," alisema Mkinga.
Alisema katika miaka hiyo mitano, Serikali imevipa kipaumbele miundombinu ya nishati na usafirishaji, Kilimo ukijumuisha na mazao ya chakula na biashara. Viwanda vinavyotumia malighafi za ndani na maendeleo ya rasilimali watu na uendeshaji wa huduma za utalii biashara na fedha.Mkinga alisema, "gharama za utekelezaji wa mpango huu ni trilioni 44.5 kwa mwaka sawa na wastani wa sh. trilioni 8.9 kwa miaka mitano. Serikali inakadiria kuwekeza trilioni 2.9 kwa mwaka wakati wastani wa trilioni 6.0 kwa mwaka zinatarajiwa kutokana na uwekezaji na wawekezaji.
Aliongeza kuwa, Serikali inategemea wananchi waamshe ukereketwa wa kimaendeleo na kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji kwa nia ya kutumia fursa hizo kupata ujuzi na kuongeza kipato kitakachochangia katika kukuza uchumi wa nchi.

No comments:

Post a Comment