29 July 2013

SHERIA ZA WAZEE KUPITIWA UPYA



Fatuma Mshamu na Revina John
TUME ya Kurekebisha Sheria Tanzania imeanza kupitia mfumo wa sheria wa huduma za jamii kwa wazee kwa nia ya kubaini udhaifu uliopo kwenye mfumo huo na kutoa mapendekezo stahiki utakaolenga ustawi na hadhi kwa kundi hilo.Ofisa Habari na Mawasiliano wa Tume hiyo, Munir Shemweta alisema wazee wanapofikia umri mkubwa uwezo wao wa kujishughulisha hupungua na kushindwa kupata mahitaji yao muhimu ya kila siku.

"Tume imeona umuhimu wa kuimarisha mfumo wa sheria kwa huduma za jamii kwa wazee ili kuwawezesha kupata huduma muhimu za maisha. Pamoja na kuwa na Sera ya Taifa ya wazee haina sheria maalumu, sheria mbalimbali za mafao zinawagusa wastaafu serikalini na sekta binafsi." alisema Shemweta.Alisema, ikumbukwe kuwa wazee hawa ni wale waliotumikia Taifa kwa nguvu na moyo wao wote kwenye ngazi mbalimbali wakati wakiwa na nguvu zao hivyo wanapokuwa wamezeeka ni muhimu kuwawekea mfumo bora wa kisheria ili kuhakikisha wanaishi maisha mazuri.
"Kwa sasa Tume inaendelea na rasimu ya awali ya kuangalia hali halisi ya Tanzania kuhusiana na suala la wazee ikiwemo mikataba ya kimataifa, mifumo ya kisheria na jamii pamoja na sera. Baada ya hapo itazunguka katika mikoa mbalimbali ili kukusanya maoni ya wazee , Ustawi wa jamii na taasii za kiserikali zinazojishughulisha na wazee", alisema Shemweta.
Katibu msaidizi na mkuu wa Kitengo cha elimu ya sheria kwa Umma, Agnes Mgeyekwa alisema wananchi wengi hawajui sheria hasa zile zinazohusu haki zao kwa ujumla, hivyo katiba mpya itakuja na mabadiliko mengi.Shemweta aliongeza kuwa ni matarajio ya tume kurekebisha sheria na baada ya kukamilika kwa mapitio ya mfumo huo wa kisheria kuhusiana na huduma za jamii kwa wazee.

No comments:

Post a Comment