MWENGE wa uhuru ulioanza mbio zake jana katika Manispaa ya Tabora
umezindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo yenye
thamani ya zaidi ya sh. bil. 2. Hayo yalibainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Suleiman Kumchaya
wakati akitoa taarifa ya miradi itakayozinduliwa katika manispaa hiyo mbele ya
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru, Juma Ali Simai.
Akisoma taarifa hiyo, Kumchaya alisema jumla ya miradi kumi na
moja ya maendeleo itazinduliwa na kuwekwa mawe ya msingi ili kuharakisha
jitihada zake za kuwaondolea kero wananchi wote waishio katika manispaa hiyo
sambamba na kuwaletea maendeleo yaliyokusudiwa.
"Ndugu zangu tumedhamiria kumaliza kero zote zinazowakabili
wananchi wetu katika wilaya hii, na huu ni mwanzo tu, ni imani yangu kuwa
jitihada zetu hizi zitafanikiwa kwa uweza wa mwenyezi Mungu kwani tumeanza
vizuri kwa mshikamano wa hali ya juu sana, ninawaombeni sana wananchi mwendelee
kutupa ushirikiano," alisema.
Miradi iliyozinduliwa jana katika mbio hizo ni nyumba ya watumishi
wa kituo cha afya Itetemia, mradi uliogharimu kiasi cha sh. mil. 82.5, mradi wa
kikundi cha vijana wajasiriamali chenye wanachama 48 ambacho kimewezeshwa
mashine 2 za kufyatulia tofali za kufungamana (interlocking bricks) zenye thamani
ya sh. 900,000 na jengo la utawala la shule ya sekondari Kanyenye lililogharimu
sh.mil.83.5.
Miradi mingine ni uzinduzi wa barabara ya Swetu yenye urefu wa km
0.997 katika Kata ya Cheyo iliyojengwa kwa kiwango cha lami kwa gharama ya sh.
mil.145.3, mradi wa kisima kirefu cha maji safi ya kunywa katika Kijiji cha
Kakurungu Kata ya Uyui kilichogharimu sh. mil. 3.4 na ujenzi wa ghala la
kuhifadhia mazao katika kijiji cha Kapunze Kata ya Ikomwa lililogharimu sh.mil.
54.
Miradi mingine ni uzinduzi wa SACCOS ya Chama cha Walimu
katika Manispaa ya Tabora yenye wanachama 411 na mtaji wa sh. mil. 480, klabu
ya wapinga rushwa katika shule ya sekondari Kariakoo yenye jumla ya wananchama
198 (wavulana 113 na wasichana 85), vikundi 7 vya akina mama wajasiriamali
ambavyo vimekopeshwa jumla ya sh. mil. 20 na mradi wa hifadhi ya msitu wa asili
Mguluko-Misha wenye ukubwa wa hekari 18 ukiwa na thamani ya sh.mil. 129.4
No comments:
Post a Comment