02 July 2013

SERIKALI YADHAMIRIA KUISIMAMIA KCBL


 Na Heckton Chuwa, Moshi
MRAJIS wa vyama vya ushirika nchini, Dkt. Audax Rutabanzibwa, amesema kuwa serikali kupitia ofisi yake itahakikisha Benki ya Ushirika mkoani Kilimanjaro (KCBL) haifi na badala yake inaimarika ili kuinua ushirika na mkulima mmoja mmoja.
Dkt. Rutabanzibwa aliyasema hayo wakati akizungumza na wanachama wa chama kikuu cha ushirika mkoani humo (KNCU) wakati wa mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika juzi mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.
"Ni vyema benki hii ikaimarishwa na zingine zianzishwe sehemu mbalimbali hapa nchini, hizi na taasisi za kifedha zinazomgusa mkulima mmoja kwa mmoja kwa vile zinaanzishwa na wakulima wenyewe kupitia vyama vyao vya ushirika," alisema.


Alivishauri vyama vya msingi pamoja na KNCU kuhakikisha wanaitumia benki hiyo kwa kukopa fedha kwenye taasisi hiyo kwa vile faida itakayopatikana itarudi kwa wanachama wake kupitia gawio.
"Serikali kwa upande wetu tutafanya kila litalowezekana kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwemo benki kuu, kuhakikisha benki hii inakua na kuimarika kwa vile inamgusa mkulima moja kwa moja na ushirika," alisema.
Aidha, Dkt. Rutabanzibwa alitahadharisha uuzwaji wa mali za kiwanda cha kukobolea kahawa kilichopo mjini Moshi cha TCCCo kwa lengo la kununua mitambo mipya ya kukobolea kahawa kutokana na iliyoko sasa hivi kuchakaa na hivyo kuathiri utendaji.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa KNCU, Bw. Maynard Swai, alisema kuwa chama hicho kikongwe barani Afrika tayari kimeilipa KCBL zaidi ya sh. milioni 150 ikiwa ni sehemu ya deni wanalodaiwa na benki hiyo.
"Ms imu wa 2 0 0 8 / 2 0 0 9 hatukupeleka malipo yoyote KCBL kutokana na mdororo wa kiuchumi ulioikumba dunia na kuiathiri KNCU kiasi cha kupata hasara ya zaidi ya shilingi milioni 800," alisema.
Katika hatua nyingine, Bw. Swai amesema kuwa chama hicho kilikusanya kilo 1,444,250 za kahawa hadi kufikia Machi 31, mwaka huu, yenye thamani ya shilingi bilioni 3.7 ambayo alisema ni asilimia 72.7 ya lengo lililowekwa la kukusanya kilo 2,000,000 za kahawa katika msimu wa 2012/2013.

No comments:

Post a Comment