02 July 2013

MADIWANI BUMBULI WATAKA SHULE MPYA KUSAJILIWA


 Na Yusuph Mussa, Lushoto

BAADHI ya madiwani wa Halmashauri ya Bumbuli wilayani Lushoto mkoani Ta n g a w ame w a t a k a wakaguzi kuzipa usajili shule nne za msingi na mbili za sekondari kwa madai wananchi wamechangia nguvu zao kujenga shule hizo.
Miongoni mwa shule hizo ni pamoja na Shule ya Sekondari January Makamba iliyopo Kata ya Milingano katika Tarafa ya Mgwashi wilayani humo.

Akizungumza mwishoni mwa wiki kwenye Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo, Diwani wa Kata ya Milingano Ramadhan Hozza alisema wananchi wametumia nguvu zao kujenga Shule ya Sekondari January Makamba na ile ya Kwalei ukiwemo mfuko wa jimbo.
"Nia ya kujenga shule za msingi ni kupunguza umbali mrefu wa kutembea watoto wetu, hivyo tunaomba Serikali itoe usajili kwa shule nne za msingi.
"Pia kwa sekondari ya January Makamba na Kwalei, Shule ya Sekondari Mbelei iwe ya kidato cha tano na sita, kwani wananchi na mfuko wa jimbo umechangia shule hizo," alisema Hozza ambaye pia ni Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Bumbuli January Makamba.


Diwani wa Kata ya Vuga, Ali Sechonge alisema umefika wakati kuacha kuongeza shule za sekondari na kujenga za ufundi, kwani kutawasaidia wanafunzi wanaoishia kidato cha nne kuweza kuwa na ujuzi na kujiajiri.
"Utitiri wa shule za sekondari ni mkubwa sana na nyingine zilijengwa kisiasa. Kama kuna uwezekano kuanzishwe shule za ufundi badala za sekondari, kwani watoto wanaomaliza kidato cha nne bado ni wadogo na hawana pa kwenda, hivyo shule za ufundi zitawasaidia kupata ujuzi," alisema Sechonge.
Kaimu Ofisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Bumbuli, Ramadhan Mkongo alisema halmashauri hiyo yenye kata 16 ina shule za sekondari 28 kati ya hizo nne ni binafsi.

Hata hivyo, kutokana na hali hiyo, aliwaomba madiwani wasiongeze shule nyingine za sekondari bali ziboreshwe zile zilizopo huku akisema Sekondari ya January Makamba itafunguliwa ikizingatia vigezo.
"Ni kweli mfuko wa jimbo pamoja na nguvu za wananchi zimetumika kujenga Shule ya Sekondari Janauary Makamba, na sisi tutapitia na kuwajulisha wakaguzi wa Kanda ya Kaskazini, lakini ni lazima tufuate utaratibu wa wizara, badala ya kujenga mpya tuboreshe zilizopo," alisema Mkongo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bumbuli, Beatrice Msomisi akijibu hoja za madiwani hao alisema Sekondari ya Mbelei kuwa ya kidato cha tano na sita alisema vigezo vya shule ya aina hiyo lazima ziwe na huduma muhimu kama maji kwa vile zitachukua wanafunzi kutoka pembe zote za nchi.
Akifunga baraza hilo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bumbuli Amir Shehiza alisema ili kupanua uchumi wa halmashauri hiyo watajenga soko na stendi kwenye miji ya Soni na Bumbuli huku wakiboresha barabara zinazounganisha vijiji, kata, tarafa na wilaya jirani.

No comments:

Post a Comment