31 July 2013

SERIKALI KUSHTAKIWA



Na Kassim Mahege

UMOJA wa Vyama vya Demokrasia Duniani(IYDU)umeungana na Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) kuitaka Serikali kuunda tume huru ili kuchunguza watu wanaohusika na machafuko nchini.Imedaiwa iwapo Serikali itashindwa kufanya hivyo itashtakiwa kwa nchi wanachama 80 wa umoja huo wanaoamini demokrasia ya kweli ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana Mwenyekiti wa umoja huo, Aris Kalafatis alisema wao wanaunga mkono suala la kuundwa tume huru ikiwa ni pamoja na kufanyika uchunguzi wa wazi ili kuweza kuwapata wahalifu ili kulinda heshima ya nchi.

"Umoja wetu utahakikisha kuwa ripoti ya machafuko tuliyopewa tunaipeleka kwa wanachama wenzetu wote duniani na kuwaita ili waweze kuiambia Serikali ya Tanzania iheshimu demokrasia," alisema Kalafatis.Mwenyekiti huyo alisema, umoja huo unaamini kuwa demokrasia ya kweli huishi na watu pasipo kutumia nguvu ikiwa ni pamoja na kutoa uhuru wa kuchagua viongozi wanaokubalika na wananchi bila vitisho.

Alisema, ripoti waliyopewa na Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA) inaonyesha kuwa Tanzania kuna ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, mauaji kwa wananchi wasiokuwa na hatia.Sambamba na vitendo vya utekaji nyara kwa watu wasiokuwa na hatia akiwemo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dkt. Stephen Ulimboka na wengine.

Alisema, mwaka 2012 umoja huo ulilaani mauaji ya mwandishi wa habari aliyekuwa akiripoti CHADEMA, Daudi Mwangosi kupitia polisi na kuongeza kuwa bado matukio hayo yanatia wasiwasi mkubwa kwa umoja huo."Umoja wetu pia umepewa idadi ya watu wasiokuwa na hatia waliotekwa ikiwa ni pamoja na mlipuko wa bomu kule Arusha na kusababisha mauaji ya watu watatu...lakini Serikali imekaa kimya," alisema Mwenyekiti huyo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa BAVICHA, Deo Munishi alisema ugeni huo umekuja hapa nchini Julai 25, mwaka huu ambapo wamepata nafasi ya kutembelea maeneo mbalimbali ili kujionea hali halisi ya nchi.

Alisema, umoja huo una vituo vyake zaidi ya 120 na washiriki kutoka nchi zaidi ya 80 duniani ambapo umejikita katika kutetea demokrasia ya kweli, haki za binadamu, siasa safi, uchumi na kupigania maendeleo.


2 comments:

  1. Hakuna ukweli wowote wa hiyo Taarifa ya IYDU inaelemea zaidi BAVICHA kupata ukweli fuatilia uione You Tube wenzao wa IYF wanavoimba na kuipongeza Tanzania 'Nakupenda Tanzania http://t.co/Jzn09Awl4b

    ReplyDelete
  2. Unapoteza muda kupigia upatu chadema. Tanzania ingelalamikiwa ingeweza kuleta vigogo wote wa dunia na kuisifia. Mnatengeneza mazingira ya serikali kutumia nguvu zaidi. Manaopotosha umma na mmefaulu kupandikiza chuki kwa wanchi. Sijui hicho chama kikiingia madarakani kitawalipa nini wananchi wanaodanganywa kila kukicha.

    ReplyDelete