Na Anneth
Kagenda
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), kimesema hakitavunja kikundi chake cha ulinzi maarufu kama Red
Brigade labda Jeshi la Polisi litangaze kuvunja kikundi cha Chama Cha Mapinduzi
(CCM)maarufu kama Green Guard.Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam juzi
na Mjumbe wa Kamati Kuu Taifa CHADEMA ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa chama
hicho, Wakili Mabere Marando wakati akihutubia mkutano wa hadhara, ulioandaliwa
na diwani wa chama hicho Kata ya Segerea, Azuri Mwambagi.
Alisema, chama chake kinaunda kikundi
cha Red Brigade kwa ajili ya kuwakabili Green Guard wa CCM na wala si polisi au
wananchi hivyo kama jeshi linaamua kwamba chama chake kisifanye hivyo basi hata
CCM isiwe na kikundi hicho."Serikali pamoja na jeshi lake
litangaze kwa umma kwamba hivi sasa linavunja kikundi hicho na sisi tutaacha
kuunda cha kwetu na kama hawafanyi, hivyo basi na sisi ni lazima tuwe na
kikundi chetu kwa ajili ya kuwakabili vijana hao wa CCM na si polisi wala
wananchi,"alisema Mwanasheria huyo.
Alisema, lengo la kuunda vikundi hivyo
ni kutokana na kiongozi mkuu wa chama hicho (CCM) kutoa maelekezo ya
kuhimarishwa kwa vikundi hivyo ili viweze kutumika nyakati za chaguzi
mbalimbali kwa kupiga viongozi wa chama chake na kusema baada ya kuona hivyo
alimwagiza Bw. Freeman Mbowe ili kuunda Red Brigade ambayo itakabiliana na
Green Guard ya CCM na si polisi.
"Katika hili tunaliambia Jeshi la
Polisi kwamba hawa wa kwetu ni kwa ajili ya kukabiliana na kikundi cha chama
pinzani na hatupo tayari kuomba radhi kwa lolote lile kwani nasi tunataka
kujilinda wenyewe,"alisema.
Alisema, wapende wasipende kikundi
hicho kitakuwepo kwani lengo lake ni zuri ambapo ni kwa ajili ya kuwalinda
CHADEMA na kukabiliana na kikundi hicho cha CCM ambacho kimekuwa kikinyanyasa
viongozi wa chama chake.
Diwani Mwambagi, akihutubia mkutano huo
kwa wananchi alisema anaunga mkono kauli ya Wakili Marando na kusema, tofauti
na hilo katika mchakato wa kuendelea kuwahudumia wananchi kwa ajili ya
kuwaletea maendeleo amekuwa akikumbana na changamoto kubwa kutokana na kwamba
hana viongozi wengi wa kusaidiana naye.
"Ndugu zangu wananchi...nyie ndio
mlionichagua lakini nimekuwa nikikumbana na changamoto nyingi mara tu
ninapoenda kuwatetea mfano kuna suala la barabara ya kilomita 1.6 lakini mita
800 ili ifike Changombe Stendi wamezikatalia lengo lao likiwa ni kutaka
kuzitumia kujinadi kwenye uchaguzi ujao kwa kununua kanga na kofia,".
"Hivyo ninawaomba tutakapo takiwa
kufanya mabadiliko ninaomba mniunge mkono kwani mita hizi nilazima zirudishwe
kwani CCM ni wanyang’anyi na ndio wanaofanya vitendo hivi," alisema
Mwambagi.
Hata hivyo, aliwazuia wananchi hao kuwa ni marufuku mwananchi yeyote
kutozwa ushuru wakati hawana soko na kwamba awali ilishatangazwa kuwa, kama mtu
hana soko hatoruhusiwa kufanya hivyo lakini cha kushangaza wananchi hao
wamekuwa wakikubali kutozwa ushuru jambo alilosema ni marufuku hadi hapo soko
katika mitaa mitano litakapojengwa.
No comments:
Post a Comment