Na Martha Fataely, Rombo
SERIKALI inaangalia upya mfumo wa utoaji zabuni za uchimbaji
wa visima kwa kuwataka watu wanaoomba kazi hiyo kufanya utafiti wa upatikanaji
wa maji katika maeneo husika. Hali hiyo inafuatia Wilaya ya Rombo kuchimba visima tisa ambapo
kati ya hivyo ni viwili pekee ndio vilitoa maji huku watu wote waliochimba
visima hivyo wakilipwa mamilioni ya fedha
. Hayo yamejiri katika ziara ya siku saba mkoani Kilimanjaro ya
Naibu Waziri wa Maji, Binilith Mahenge ambapo alisema Serikali imechimba visima
zaidi ya 1,800 nchini na kupata maji kwa asilimia 69 tu. Alisema Serikali imekuwa ikipata hasara kutokana na watu hao
kulipwa fedha huku visima hivyo vikibaki bila kuhudumia jamii iliyokusudiwa
hivyo ni vyema mfumo huo kutizamwa upya.
Awali katika taarifa yake kwa waziri huyo, Mhandisi wa maji wa
Wilaya ya Rombo, Andrew Tesha alisema katika mradi wa programu ya maji na usafi
wa mazingira vijijini tayari visima tisa katika vijiji vya wilaya hiyo
vimechimbwa. Alivitaja vijiji hivyo kuwa ni Ngoyoni, Ngareni, Mahorosho,
Msaranga, Shimbi Mashariki, Leto, Kiraeni, Urauri na Kahe kila kimoja kikiwa na
kina cha urefu wa zaidi ya mita 140.
"Kati ya vyote hivi vijiji vitano havikutoa maji kabisa huku
viwili vikitoa maji na kushindikana kutokana na kuporomoka kwa miamba huku vile
vya Leto na Kahe vikitoa maji ambayo yanatarajiwa kutumiwa," alisema
Tesha. Alisema kazi hiyo ilifanikiwa kwa kisima cha Kahe ambacho kina
uwezo wa kuzalisha wastani wa lita 10,285 kwa saa huku kile cha Leto kimetoa
wastani wa lita 3,600 kwa saa maji ambayo ni kidogo hivyo kisima cha Kahe pekee
ndicho kimeingia kwenye mchakato wa kuendelezwa.
Naye Mkurugenzi
mtendaji wa halmshauri ya Wilaya ya Rombo, Tadeus Mboya alisema baada ya
kukosekana kwa maji katika visima hivyo vilivyochimbwa katika vijiji hivyo
walilazimika kutafuta vyanzo vingine vya maji na kuhakikisha wananchi wa maeneo
husika wanapata maji.
No comments:
Post a Comment