29 July 2013

MAPAMBANO VVU KWA WATUMISHI YATAPUNGUZA MAAMBUKIZO NCHINI



Na Suleiman Abeid
ATHARI za UKIMWI katika jamii ni kubwa ikiwemo kupunguza uzalishaji kwa kupoteza nguvukazi.Zaidi ya asilimia sabini ya wanaoambukizwa na kuugua UKIMWI ni watu wenye umri kati ya miaka 20 hadi 40 ambao ni vijana. Kundi hilo ndilo linalotegemewa na familia na taifa kwa ujumla katika maisha, utendaji, uzalishaji mali na hali ya baadaye ya Taifa.

Hivyo, ni lazima tuupige vita UKIMWI kwa nguvu zetu zote. Tuanze kwa kuzuia maambukizo kwa wale karibu asilimia 85 ya watu wazima ambao hivi sasa hawana virusi vya UKIMWI, ili wabakie katika hali iliyo salama.VVU ni tatizo kubwa la maendeleo linaloathiri sekta zote. Katika kipindi cha miongo miwili iliyopita umeenea bila huruma na kuathiri watu katika nyanja zote za maisha na kuangamiza sehemu kubwa ya watu wanaoshiriki katika uzalishaji mali hususan wanawake na wanaume wenye umri kati ya miaka 20 hadi 49.
Maneno hayo yalitamkwa na Rais wa awamu ya tatu hapa nchini, Bw.Benjamin Mkapa mwaka 2002 alipokua akizindua rasmi sera ya UKIMWI nchini ambapo aliutangaza ugonjwa huo kama janga la Taifa na kuwaomba Watanzania wa rika zote kushiriki kikamilifu katika vita dhidi ya ugonjwa huo.Sera hiyo ya UKIMWI inaeleza kwamba serikali kwa upande wake ina wajibu wa kusimamia na kuongoza masuala ya fedha katika shughuli za Taifa kuhusu uambukizo wa VVU na kwamba katika kipindi hicho ilitenga dola za Marekani milioni nane kwa ajili ya shughuli hizo.
Hata hivyo kutokana na serikali kutokuwa na fedha za kutosha ilielekeza wadau wengine ikiwemo idara zake, taasisi za umma, halmashauri za majiji, manispaa, miji na wilaya na zile za binafsi kushiriki kikamilifu katika mapambano hayo.Lengo kubwa ni kila mtu kushiriki katika mapambano dhidi ya maambukizo ya virusi vinavyosababisha ugonjwa hatari kwa kuwezesha kupunguza idadi ya maambukizo mapya miongoni mwa jamii.
Kutokana na hali hiyo idara na taasisi mbalimbali za serikali na mashirika ya kidini zimejitosa katika vita hiyo kupitia semina na makongamano mbalimbali ikiwemo uhamasishaji wa upimaji kwa hiari.Idara ya Uhamiaji nchini katika kuunga mkono wito wa serikali hivi sasa imeanzisha zoezi la upimaji wa hiari kwa watumishi wake nchi nzima sambamba na kutoa elimu kwa wateja wake mbalimbali wanaokwenda katika ofisi zake kutaka huduma mbalimbali.
Kamishna msaidizi wa uhamiaji nchini, Bi.Salome Kahamba anasema, katika kukabiliana na wimbi la maambukizo mapya ya VVU miongoni mwa watumishi wa idara hiyo, wameanzisha zoezi la upimaji wa hiari kwa watumishi wake ili kuweza kuwasaidia wale wote watakaobainika kuambukizwa virusi hivyo.
Anasema, hilo litahusisha pia familia za watumishi hao kwa vile pindi itakapotokea mmoja wa watu wanaoishi na mtumishi akaugua UKIMWI kwa njia moja ama nyingine mtumishi huyo atalazimika kumshughulikia kwa kipindi kirefu na hivyo kujikuta akishindwa kutimiza vizuri majukumu yake ya kikazi.
“Idara yetu ya Uhamiaji mnamo mwaka 2003 tulikaa chini na kutafakari janga hili la UKIMWI hapa nchini, tukaona hata sisi tusipojitosa kupambana nalo linaweza kuwa na athari kubwa katika utendaji wa idara yetu,
“Tuliamini wazi kwamba tukizembea, tutapoteza kwa kiasi kikubwa nguvukazi ya idara kwa watumishi wetu wengi kupukutika kwa gonjwa hili, hivyo tuliona ni vyema tuunge mkono juhudi za serikali katika kupambana na maambukizo ya virusi vya UKIMWI kama alivyotangaza Rais mstaafu Bw. Benjamin Mkapa,” anasema Bi. Kahamba.
Bi. Kahamba ambaye pia ndiye mratibu wa kudhibiti maambukizo mapya katika idara hiyo ya uhamiaji anasema, ili kuhakikisha vita dhidi ya maambukizo mapya inafanikiwa, idara iliwapeleka nchini Uganda baadhi ya watumishi wake ili kwenda kujifunza mbinu za ushauri nasaha.
Anasema, mpaka hivi sasa tayari wana washauri nasaha waliopata mafunzo watumishi 35 na pia waelimishaji rika 70 ambao watasambazwa katika mikoa yote nchini kwa ajili ya kufanya kazi ya uhamasishaji na ushauri nasaha utakaowezesha watumishi wote kupima kwa hiari ili kuelewa afya zao.
“Janga hili tusipolivalia njuga linaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa uchumi wa nchi na ndiyo maana idara yetu mbali ya kuendesha zoezi la upimaji wa hiari kwa watumishi wake, lakini pia tumeanza kuweka bajeti maalumu kwa ajili ya kuwasaidia watumishi ambao watabainika kuwa wameambukizwa VVU,
“Na huduma hii si lazima itolewe kwa mtumishi tu, hata kama mtumishi atakuwa hajaambukizwa VVU lakini labda mkewe, mtoto au mtumishi wa ndani anayeishi naye akiwa ameambukizwa pia huyu atapatiwa huduma zote muhimu anazopaswa kupatiwa mtu mwenye VVU,”anasema Bi. Kahamba.
Anasema kutokana na hali hiyo wanahimiza watumishi kuhakikisha wanapimwa pamoja na familia zao na kwamba kitendo cha mtumishi kutowapeleka watu wanaomtegemea katika huduma ya upimaji kinaweza kuathiri bajeti ya idara pale itokeapo mtumishi huyo kubaini ana mtu anayeugua UKIMWI.
“Tumewasisitiza watumishi wetu wahakikishe kwamba hata watu wanaoishi nao wanapimwa ili waweze kufahamu afya zao hii ni pamoja na watumishi wa ndani, hawa ni muhimu sana, maana ndiyo wanaobaki wakiwalelea watoto wao majumbani.”
Anasema, mbali ya kuendesha zoezi la upimaji wa hiari kwa watumishi pia idara imekuwa ikitoa vipeperushi na mabango yenye maandishi yanayotahadharisha juu ya athari ya UKIMWI na jinsi ya kujikinga na maambukizo mapya.
Kwa upande wake mmoja wa washauri nasaha katika idara hiyo ya uhamiaji, Bw.Justus Kusiluka anasema suala la mtu kupima afya yake kwa hivi sasa ni muhimu sana kwa vile ataweza kuishi bila hofu kila wakati na anakuwa na uhakika wa kupanga mipango yake ya maisha vizuri.
Bw. Kusiluka anasema, wapo baadhi ya watu ambao hawapendi kupima afya zao lakini wamekuwa wakiishi kwa hofu kubwa pale inapotokea kuugua homa mara kwa mara na hivyo kuhisi tu kwamba wameambukizwa.
Anasema, “Ni muhimu kupima, usipopima unasababisha mtu uishi maisha ya hofu, daima unakuwa na wasiwasi, lakini pia unashindwa kupanga mipango yako vizuri, ni vizuri tukatumia hiari tuliyonayo katika kupima,”
“Kama hujapima unapougua gonjwa lolote lile, tayari unakuwa na wasiwasi, labda nimeathirika, lakini kwa wale walioathirika wataweza kuelewa jinsi ya kuishi kwa matumaini na mtu anapata maelekezo ya mpangilio wa lishe yake iweje, hivyo ataishi maisha marefu kama wengine.”

No comments:

Post a Comment