04 July 2013

SERIKALI KUPAMBANA NA VIGOGO WANAOJIHUSISHA NA UHARAMIA


 Kassim Mahege na
Rehema Maigala
SERIKALI itahakikisha inapambana na maharamia dhidi ya wanyamapori ikiwa ni pamoja na watu wote wanaotoa fedha kwa lengo la kusaidia vitendo vya kijangili, bila kujali nyadhifa zao wala madaraka waliyokuwa nayo nchini.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Utalii Lazaro Nyalandu wakati alipotembelea katika Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba Jijini Dar es Salaam jana kuwa wizara yake itahakikisha inawakamata Wakubwa wanaofadhili ujangili duniani kote. “Kupitia mfumo wa Air Transport Infrastructure, kwa kushirikiana na Serikali ya watu wa Marekani, tutawakamata vigogo wote duniani wanaodhamini Ujangili,”alisema Nyalandu.

Akifafanua zaidi alisema zamani maharamia hao walikuwa wakishughulika zaidi na Pembe za ndovu na kuongeza kuwa sasa hivi wamewageukia Simba ambapo inaaminika kuwa ukipata moyo wake utatajirika, jambo ambalo sio sahihi.

Alisema Sekta ya Utalii ndio sekta inayotoa ajira nyingi zaidi hivyo Serikali itahakikisha inawakamata maharamia hao hata kama watatumia magari makubwa (Fuso) yenye namba za Serikali.
Alisema hivi sasa kuna ujangili wa wanyamapori na kuongeza kuwa katika Mkoa wa Dar es Salaam wapo watu hao hivyo watapambana nao usiku na mchana ili kuwatia mikononi mwa vyombo vya dola.

“Sekta ya utalii mwaka jana imechangia asilimia 17 katika pato la Taifa na ndio sekta pekee inayoingiza pesa nyingi za kigeni, hivyo hatuwezi kuwaachia maharamia watawale katika sekta hiyo,”alisema Nyalandu.
Alisema mwaka jana idadi ya watalii ilikuwa 1.1 milioni na kuongeza kuwa mwaka huu malengo yao ni kufikisha idadi ya watalii milioni mbili.
Alisema anapenda kuwasihi Watanzania wenye tabia hiyo kuacha mara moja kwani atakayefanya vitendo vya ujangili lazima atakamatwa.

No comments:

Post a Comment