Na Penina Malundo
WAZIRI wa
Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amesema ifikapo Julai 2014, mradi
wa kulaza bomba la gesi umbali wa kilomita 534, kutoka Mtwara hadi Dar es
Salaam, utakuwa umekamilika.
Alisema bomba hilo likifika Dar es Salaam,
litasambazwa katika mikoa mbalimbali nchini ili Watanzania wengi ambao hawana
umeme waweze kuipata nishati hiyo hasa maeneo ya vijijini.Profesa Nuhongo
alisema hayo Dar es Salaam jana katika kongamano la wazi ambalo lilikuwa
likijadili na kupokea maoni mbalimbali kutoka kwa wadau wa nishati juu ya
miradi mikubwa ya kitaifa kwenye sekta ya nishati na madini.
"Naamini
mradi huu ukikamilika, utaweza kuwanufaisha Watanzania wengi hasa waishio vijijini
kupata umeme wa uhakika... hatutaangalia wingi wa vijiji mikoani bali
tutaangalia wingi wa watu," alisema Prof. Muhongo.
Aliongeza kuwa,
kuna tetesi zinazodai Wachina ndio wahusika wa kusambaza bomba hilo jambo
ambalo halina ukweli, bali Serikali ya nchi hiyo imeikopesha Tanzania dola za
Marekani bilioni 1.2 ambapo deni hilo linatarajiwa kuisha ndani ya miezi 18.
"Mradi huu
ni wa Watanzania si Wachina kama inavyosemwa na baadhi ya watu hasa hivyo
wananchi...njia mojawapo ya kuifanya nchi yetu iwe na maendeleo kiuchumi ni
pamoja na gesi ambayo itatupa fursa ya kuiuza nchi jirani," alisema.
Hata hivyo,
Prof. Muhongo alibainisha kipaumbele cha Serikali katika miradi ambayo
itatekelezwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo na njia saba mpya za umeme
wa msongo wa juu.
Alisema njia hizo zitakuwa na umbali wa
kilomita 3,000 ambapo mfumo mkuu wa kusafirishia umeme huo utaanzia katika
Mikoa ya Dar es Salaam-Arusha, Singida-Arusha, Somanga- Kinyerezi pamoja na
Makambako hadi Songea.
Aliongeza kuwa, awamu ya kwanza ya ujenzi
wa njia ya kusafirishia umeme Kaskazini- Magharibi, itaanza katika Mikoa ya Dar
es Salaam na Dodoma.
Prof. Muhongo alisema miradi hiyo
itaongeza kasi ya upatikanaji umeme mijini, vijijini na kuweza kuwafikia
Watanzania milioni tano sawa na asilimia 30 ya wananchi wote ifikapo 2016.
Alisema mwaka 2012-2013 Watanzania
wanaotumia umeme nchini ni asilimia 21 ambapo mwaka 2005, walikuwa asilimia 10
ila kwa makisio ya haraka, mwaka 2015 watumiaji nishati hiyo wataongezeka
kutoka asilimia 21 hadi 30.
Aliongeza kuwa, nchi zenye uchumi mkubwa katika
Bara la Ulaya, zinategemea sana uchumi wa nishati mbadala ambao huuza katika
baadhi ya nchi jirani na kuongeza pato lao kiuchumi.
mipango mingi, utekelezaji ndio tatizo unagubikwa na ufisadi
ReplyDelete