30 July 2013

POULSEN AJITETEA KIPIGO UGANDA



Na Fatuma Rashid
KOCHA Mkuu wa Timu ya Taifa Stars, Kim Poulsen amejitetea kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Uganda 'The Cranes' kuwa kilitokana na wachezaji wake wengi kuwa katika mfungo wa Ramadhani.Katika mechi hiyo ya kuwania kucheza fainali za Wachezaji Wanaocheza Ligi za Ndani (CHAN), ilichezwa Uwanja wa Mandela, ambapo katika mechi ya kwanza iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Stars walifungwa bao 1-0.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Poulsen alisema kuwa amehuzunika sana na kipigo hicho ingawa mfungo ulichangia lakini hatakata tamaa.Alisema kuwa wachezaji walijipanga walicheza vizuri, lakini ili mchezaji afanye vizuri anatakiwa apate chakula na maji ya kutosha ila kutokana na mfungo ilichangia timu hiyo kutofanya vizuri. 
"Kufunga pia kulichangia timu kufungwa wachezaji walipungukiwa nguvu, pia kukosekana kwa wachezaji Mwinyi Kazimoto na Shomari Kapombe kulileta pengo kubwa," alisema Kim.Aliongeza kwa sasa ana muda mrefu wa kukiandaa kikosi chake vizuri hivyo Watanzania wasikate tamaa.Alisema kuwa kuna haja ya kuwaendeleza wachezaji Vijana ili kuweza kuandaa wachezaji watakaoweza kuchezea timu ya Taifa.
Pia kocha huyo aliahidi kuwa Watanzania wataona mabadiliko makubwa hapo baadaye, kwani anaamini kutokana na makosa madogo madogo aliyoyaona kwa baadhi ya wachezaji yanarekebishika.
"Umoja ni nguvu katika kila jambo na tukishirikiana najua tutafanya vizuri,timu inapokuwa na mafanikio lazima kuna kipindi inakwama na ndivyo ilivyotokea katika timu yangu lakini inabidi tuangalie timu ilipotoka na inapoelekea," alisema.Poulsen aliongeza kuwa hivi sasa timu hiyo inajiandaa na mechi yake dhidi ya Gambia kukamilisha ratiba yao katika michuano ya kuwania kucheza Kombe la Dunia.

No comments:

Post a Comment