Na Mashaka Mhando, Tanga
MFUKO wa Taifa wa
Hifadhi ya Jamii (NSSF), unaandaa utaratibu wa k uwa k o p e s h a wanachama
wake sehemu ya michango yao wanayolipa kila mwezi ili kuwasaidia kuboresha
maisha na kupambana na umaskini.
Sanjari na hilo, mfuko huo umewataka wananchi nchini kubadili
mitizamo yao ya kuchangia harusi na sherehe mbalimbali za kijamii na badala
yake wawekeze sehemu ya fedha wanazozipata, katika mifuko ya hifadhi ya jamii.
Akizungumza katika semina ya siku tatu kwa Jumuiya ya Wanawake
nchini (UWT) inayofanyika jijini Tanga, Meneja wa NSSF Mkoa wa Tanga, Frank
Maduga alisema kuwa mfuko huo unaandaa utaratibu utakaowawezesha wanachama
kukopeshwa fedha kukidhi mahitaji yao.
"Wadhamini wa mfuko wanaandaa utaratibu ambao utawawezesha
kukopa kile wanachochangia kila mwezi, hii itawasaidia wanachama wetu kuona ni
namna gani wanaweza kupambana na umaskini," alisema Maduga.
Alisema wananchi hapa nchini lazima wafahamu maisha yamekuwa na
changamoto nyingi hivyo suala la kuhifadhi fedha katika mifuko ya jamii ni
suala la kisheria ambalo wanatakiwa walipe kipaumbele kwa ajili ya kuwasaidia
hapo baadaye.
"Wananchi lazima waweke kipaumbele katika suala la akiba kwa
maisha ya baadaye...Hii michango ya harusi wanayojali zaidi haina faida wajue
maisha yamekuwa na changamoto nyingi kwa sasa ni bora wakajali na kuwekeza
katika mifuko ya jamii," alisema Maduga.
Hata hivyo alikemea tabia ya jamii ya watu wa Mkoa wa Tanga kila
inapofika wakati wa sikukuu na mwanzoni mwa mwaka, wanajitoa kuchangia katika
mfuko huo na kuchukua fedha zao kwa ajili ya matuminzi ya wakati huo akieleza
kwamba hayana faida.
Alisema ni vyema wananchi wakaendelea kuchangia kwa faida ya
baadaye kuliko kuchangia kisha kuchukua fedha hizo kwa lengo la kujitoa akieleza
kwamba matokeo yake, hawawezi kujiwekea akiba ya mbeleni.
Miongoni mwa wajumbe katika semina hiyo, Mbunge Viti Maalum
Singida, Martha Mlata alisema mafunzo hayo yametolewa muda mwafaka kwani
yameweza kuwajenga kisiasa.
Alisema kuwa watahakikisha wanakwenda kuhamasisha wanachama
ili waone umuhimu wa kujiunga na mfuko huo, kuweza kupata mafao ya uzeeni
sambamba na matibabu pindi wanapougua.
No comments:
Post a Comment