29 July 2013

MRADI WA KILIMO WAENDESHWA KIFAMILIA



 Na Mashaka Mhando, Korogwe
MKUU wa Wilaya ya Korogwe, Mrisho Gambo ameshikilia msimamo wake wa kusimamisha utekelezaji wa mradi wa kilimo cha umwagiliaji Kwamkumbo wenye gharama ya shilingi milioni 220 akidai taratibu nzima za ujenzi hazikufuatwa huku sura ya mradi ikionekana kuwa ni ile ya kifamilia.
Gambo alionyesha msimamo wake huo mwishoni mwa wiki alipokuwa ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Luteni mstaafu Chiku Gallawa aliyefanya ziara yake kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani Korogwe ambapo pia alipata fursa ya kuzungumza na wakulima wa skimu za kilimo cha umwagiliaji.
Akiwa katika mkutano na wakulima wa skimu ya umwagiliaji Mombo, Gambo alisema "Mradi nimeusimamisha hadi pale taratibu zitakapofuatwa, kamati yote inaonekana ni ya kifamilia.. shemeji, mke na mume na watoto huku taratibu, kanuni na sheria za kutoa zabuni ya ujenzi hazikuweza kuzingatiwa."
Mbali na kuyasema hayo Gambo alikwenda mbali zaidi kwa kuwaasa baadhi ya wana CCM wanaolishabikia suala hilo la kusimamishwa kwa mradi wakilieleza tofauti hatua ambayo imekuwa ikizusha manung'uniko miongoni mwa jamii jambo alilosema siyo vyema kuendelea kwa mradi kwa watu hao wa familia moja.
"Mimi ninachotaka kusema ni kwamba lazima kanuni, sheria na taratibu zifuatwe pale, labda niwaase wanaCCM wanaolishabikia jambo lile wangejaribu kuuliza wapate majibu sahihi siyo vyema kushabikia mambo tu," alisema Gambo.
Licha ya kuyasema hayo mkuu huyo wa wilaya alisisitiza msimamo wake wa kanuni, taratibu na sheria kufuatwa ndipo mradi huo uweze kufanyiwa kazi ambapo awali kiongozi huyo kabla ya mkuu wa mkoa kufika aliweza kuutembelea mradi na kujionea mapungufu kadhaa yenye kuashiria mazingira ya ufujaji wa fedha kwa kikundi cha watu wachache.
Akizungumza katika mkutano huo, mkuu wa mkoa wa Tanga, Gallawa aliagiza watu waliokiuka sheria kwenye shughuli za ujenzi wa mradi huo kuchukuliwa hatua zinazostahili huku naye akiwaasa wananchi kutokubali kushirikishwa kwenye mbinu zinazoashiria mazingira ya uchafu.
Aidha aliwataka watumishi kufanya kazi kwa kujituma huku wakizingatia nidhamu na maadili kwa maelezo kuwa kufanya hivyo ni sawa na ibada inayotosheleza kwa mwenyezi Mungu hatua ambayo pia itasaidia upatikanaji wa maendeleo ya haraka kwa wananchi walio wengi.
Sakata la kusimamishwa kwa matumizi ya fedha za skimu ya umwagiliaji Kwamkumbo liliibuka katika siku za hivi karibuni ambapo ofisa kilimo na umwagiliaji na wote waliokuwa wakihusika na uendelezaji wa mradi huo walitakiwa kusitisha matumizi ya fedha hizo hadi taratibu za sheria zitakapofuatwa

No comments:

Post a Comment