26 July 2013

MKANDARASI AAHIDI KUTEKELEZA AHADI YA MAGUFULI



 Na Habib Miradji
MKANDARASI anayejenga kipande cha barabara ya Ndundu hadi Somanga , inayounganisha mikoa ya Pwani na Lindi, kampuni ya MA Kharafi, amesema amejipanga kumaliza kazi za ujenzi wa mradi huo kama alivyoelekeza Waziri wa Ujenzi, Dkt. John Magufuli.Amesema atafanya hivyo iwapo ataendelea kupata ushirikiano kutoka kwenye mamlaka mbalimbali Serikalini zinazohusiana na utekelezaji wa mradi huo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mkandarasi huyo kwenye eneo la mradi hivi karibuni mara baada ya ziara ya waziri Dkt.Magufuli, ilisema ufuatiliaji wa waziri huyo umewapa matumaini mapya ya kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo kabla ya Desemba 30,2013.Alisema hatua hiyo itafikiwa iwapo waziri huyo atasaidia kuhimiza wadau wengine muhimu kutekeleza majukumu yao kwa wakati yakiwemo malipo wanayodai.
T a a r i f a h i y o i n a t a j a ucheleweshwaji wa malipo kuwa umesababisha mkandarasi kutumia zaidi ya sh. bilioni 20 wakati wa kipindi cha kusimama mradi huo kwa kulipa mishahara wafanyakazi wake na gharama za uendeshaji wakati wa kusubiri malipo.
“Ucheleweshwaji wa malipo unasababisha hasara pia kwa Serikali kulipa fedha nyingi zaidi kuliko gharama za awali za mradi huo,” ilieleza sehemu ya taarifa yake.
Taarifa hiyo ilibainisha kuwa moja ya mikakati ya kujizatiti kukamilisha mradi huo ni kuongeza magari na mitambo ambapo hivi karibuni wamenunua malori makubwa aina ya tipa 13 kwa ajili ya kukamlisha kazi mapema.
Ilisisitiza kuwa malimbikizo ya malipo wanayodai yakipatikana kwa wakati watanunulia mafuta ya kuendeshea mitambo hiyo na kuifanyia matengenezo mitambo iliyoharibika.
“Mkandarasi si mfadhili wa mradi, anapofanya kazi alipwe mara moja ili kazi nyingine ziendelee vinginevyo kazi lazima zisimame na gharama kuongezeka,” ilieleza taarifa hiyo. Ilidaiwa kuwa kutokana na usumbufu wanaoupata wangeweza kuvunja mkataba, lakini mahusiano mazuri na serikali, ushirikiano, Dkt. Magufuli na Mkurugenzi Wakala wa Barabara (TANROADS) Patrick Mfugale, ndio imemfanya kuendelea kuvumilia hadi watakapomaliza mradi huo.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa Wizara ya Fedha haijaidhinisha maombi ya mkandarasi huyo ya misamaha ya kodi kwa ajili ya ununuzi wa mitambo uliofanywa na mkandarasi tangu mwaka 2011 hadi 2013.Misamaha ambayo ipo kwenye mkataba ni msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa ajili ya ununuzi wa mafuta ya dizeli.
Mradi wa ujenzi wa sehemu ya barabara hiyo ukikamilika utaunganisha Jiji la Dar es Salaam na mikoa ya kusini ambapo ulisainiwa Juni 30, 2008 kati ya Serikali na kampuni ya MA Kharafi.Thamani ya mradi ilikuwa sh. bilioni 58.8. Awali mradi ulipangwa kukamilika Januari 14, 2011 lakini kutokana na sababu mbalimbali zilizo nje ya mkandarasi serikali ililazimika kumwongezea muda ili kukamilisha kazi hiyo Desemba 30, 2013

No comments:

Post a Comment