KITUO cha Maendeleo ya Viwanda mkoani Kilimanjaro
(KIDT), kimekarabati Tanuru la kuchoma Insulator katika kituo kidogo cha Wilaya
ya Same kwa zaidi ya sh milioni 30 lengo likiwa ni kuongeza uzalishaji wa
bidhaa hizo ambazo zinauhitaji mkubwa hapa nchini na nchi jirani.
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Meneja Mkuu
wa KIDT, Mhandisi Frank Elisa alisema pamoja na kukarabati tanuru hilo bado
wanauhitaji wa matanuru mengine mawili ili kuweza kukabiliana na changamoto
kubwa ya uhitaji wa bidhaa hizo hapa nchini.
Mhandisi Elisa alisema kukarabatiwa kwa tanuru hilo
kumeongeza uzalishaji wa Insulator kutoka 10,000 zilizokuwa zikizalishwa mwanzo
hadi kufikia insulator 25,000 hivyo kupunguza tatizo la uhitaji wa bidhaa hizo.
"KIDT tunakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo
upungufu wa matanuru na tunaendelea kukkabiliana nazo ili kuhakikisha
tunazalisha bidhaa nyingi ambazo zitatosheleza hapa nchini na Afrika Mashariki
kwa ujumla," alisema.
Katika hatua nyingine meneja huyo aliishauri serikali
kupitia wizara ya viwanda, kuvilinda viwanda vilivyopo katika maeneo mbalimbali
hapa nchini na kuhakikisha vinafanya kazi kwa ufanisi, hatua ambayo itasaidia
kuleta mabadiliko ya kimaendeleo na kukuza uchumi wa nchi.
Alisema kuna haja ya Serikali kuvilinda viwanda
vichache vilivyopo na mabavyo vinafanya kazi na kuhakikisha inaviongezea mtaji
ili kuweza kuleta mabadiliko ya kimaendeleo na kukuza uchumi kupitia sekta ya
viwanda hapa nchini.
Pia alisema Serikali imeonekana kuvisahau viwanda;
hali ambayo imesababisha viwanda vingi kujiendesha kwa fedha za wateja hivyo
kujikuta vikifanya kazi kwa kusuasua na kushindwa kuchangia mabadiliko ya
kimaendeleo na kukuza uchumi wa nchi kama ilivyokusudiwa.
"Tunaiomba serikali ivilinde viwanda vya ndani na
kuviongezea mtaji, kwani kwa sasa sisi wenyewe tunajiendesha kwa fedha za
wateja na wakichelewa kulipa tunashindwa kuendelea mbele," alisema.
Kwa upande wake msimamizi wa Kituo cha KIDT wilayani
Same ambacho kinahusika na utengenezaji wa Insulator na vyombo vya udongo na
jamii yake, Loveness Mhina alisema, hali ya uzalishaji wa Insulator kwa sasa ni
mzuri ikilinganishwa na kipindi cha nyuma.
Alisema pamoja na uzalishaji kuwa mzuri bado
wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa matanuru ya kuchoma
insulator na Shirika la Umeme nchini TANESCO kuchelewa kulipa fedha mara baada
ya kuchukua insulator.
"Bidhaa yenye soko kubwa sasa ni Insulator ambazo
huchukuliwa kwa oda na TANESCO lakini TANESCO huchelewa kulipa fedha, hali hii
husababisha tushindwe kuendelea mbele kutokana na kukosa fedha za
kujiendesha," alisema.
Aidha, alisema ni vema serikali ikaangalia uwezekano
wa kuwaongezea matanuru mengine mawili katika kituo hicho, hatua ambayo
itawawezesha kuzalisha bidhaa nyingi zaidi na kufanikisha jitihada za Serikali
za kukuza ajira hapa nchini.
No comments:
Post a Comment