Na Mwajabu Kigaza, Kigoma
KUKITHIRI kwa migogoro
ya ardhi katika Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma inayosababishwa na
baadhi ya viongozi wa Manispaa hiyo imekuwa chanzo cha wananchi kukatana
mapanga wakati wa maziko katika eneo la Bushabani lililopo katika Kata ya
Kibirizi mkoani hapa
. Katibu wa Chama cha NRA Taifa, Hamisi Kiswaga ameamua
kulishughulikia tatizo hilo ambalo lina muda mrefu bila kupatiwa ufumbuzi
katika kata hiyo ambapo zaidi ya maiti tano kwa nyakati tofauti zilizuiliwa
kuzikwa katika eneo la maziko na hivyo kulazimika kuzika chini ya usimamizi wa
polisi kutokana na mgogoro wa ardhi.
Kiswaga alisema kuwa, amekuwa akipokea malalamiko ya wakazi wa
eneo hilo kuzuiliwa kuzika kwenye makaburi yaliyopo katika mtaa wa Bushabani
kwa kipindi cha mwaka huu jambo ambalo linazua balaa ambapo makaburi hayo
yalikuwa yakitumika tangu mwaka 1987.
Aidha aliitaka Idara ya Mipango miji kutatua mgogoro huo wa sehemu
ya kuzikia ya maiti katika mtaa huo ili kuepusha maafa yanayoweza kujitokeza
kutokana na baadhi ya wakazi kudai kuwa eneo hilo ni lao na kusababisha wakazi
wa eneo hilo kuzika maiti zao kwa usimamizi wa askari polisi.
Wakizungumzia jambo hilo kwa nyakati tofauti, Mwenyekiti mstaafu
wa mtaa wa Bushabani, Haruna Bakunda na Lulinda Mustafa walisema kuwa chanzo
cha vurugu hizo ni Mama Senga na familia yake ambao wanadai eneo hilo ni lao
walilorithi toka kwa marehemu baba yao ambaye alikuwa mtawala wa eneo hilo enzi
za ukoloni.
"Kero hii imekuwa ya muda mrefu na malalamiko yamefikishwa katika
uongozi wa Manispaa pamoja na polisi, lakini hakuna hatua zilizokuwa
zikichukuliwa ndiyo tukaamua kuonana na viongozi wa NRA ili watupatie msaada wa
kutatua kero hiyo ambapo mama huyo na watoto wake wamekuwa tishio katika eneo
hilo.
"Hivi karibuni limetokea sakata la kichapo hadi mtu mmoja
kalazwa katika Hospitali ya Maweni kisa ni kukataza kuzika katika eneo hilo la
makaburi, hii ni kero tunataka kuwa huru katika mazishi na sio kusimamiwa na
polisi," alisema Mwenyekiti huyo mstaafu.
Akitoa majibu katika kikao maalumu na viongozi wa Chama cha NRA,
wakazi wa eneo la Bushabani, Meya, OCD mbele ya Kaimu Mkurugenzi, Naibu meya wa
Manispaa hiyo, Yunusi Ruhomvya alisema kuwa kwa mujibu wa sheria eneo hilo lipo
kwa lengo la maziko na kuwataka wananchi hao wawe wavumilivu ili wapatiwe
majibu yaliyo sahihi kutoka kwa viongozi wa mipango miji watakapomaliza kikao
chao.
"Keshokutwa mtapata majibu
sahihi kuhusu eneo hili, ikiwa ni pamoja na kupata ramani ya eneo hilo na
kuondoa kero hiyo ambayo imekuwa ya muda mrefu," alisema Meya huyo..
No comments:
Post a Comment